Alisema hayo wakati wa mkutano uliowakutanisha Baraza la Wazee wa CCM Mkoa wa Dodoma na Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Chiku Gallawa.
“Mazuri ya Serikali ni mengi sana ni lazima yasemwe Serikali ya Chama
Cha Mapinduzi (CCM) imefanya mengi mazuri lakini hayasemwi, ifike
wakati mazuri ya Serikali lazima yasemwe. “Kama kuna mtu ambaye anadhani
serikali haijafanya lolote katika kuwaletea wananchi wake maendeleo
huyo atakuwa ana lake jambo ” alisema Ndejembi.
Mzee Ndejembi alisema serikali ya CCM imefanya mambo mengi makubwa na
mazuri katika nchi hii, ambayo kila mtu anatakiwa kujivunia akitaja
barabara kama moja ya mafanikio kutokana na mitandao yake kuunganisha
mikoa hadi wilayani.
Mzee Ndejembi ambaye amewahi kushika nyadhifa mbalimbali katika
kipindi cha uongozi wa Mwalimu Nyerere, anasema kukaa kimya watu
wakiisimanga serikali ya CCM haijafanya kitu ni uwoga usiokuwa na
msingi.
Alisema taifa hili limepiga maendeleo makubwa katika sekta ya elimu,
afya, mawasiliano na demokrasia na hayo lazimwa yasemwe wazi.
Katika mkutano huo naye Balozi mstaafu, Job Lusinde amesema kuna
mambo mengi yamefanywa na serikali na kila mtu anatakiwa kutambua hilo.
Lusinde ambaye aliwahi kuwa Waziri wa kwanza katika Baraza la
Mawaziri wa serikali ya kwanza ya Tanganyika baada ya Uhuru mwaka 1961,
alisema serikali ya CCM imefanya mengi ambayo yanatakiwa kupongezwa.
Mkuu wa Mkoa alisema kwamba watahakikisha wanatangaza mafanikio ya
serikali mkoani hapa, kutokana na ukweli kuwa serikali imewekeza sana
mkoani humo lakini mengi hayasemwi.
Anasema kama mkoa wamejipanga kutangaza mambo yote ambayo serikali
imefanya mkoani Dodoma kupitia televisheni, redio na magazeti.
Mmoja wa wajumbe wa baraza hilo, Dk Bright Mbaga anasema serikali ya
CCM inapaswa kupongezwa kwa maendeleo yaliyopo sasa nchini katika nyanja
za elimu, afya, miundombinu na mengineyo.
Anasema licha ya mkoa kuwa na changamoto mbalimbali, lakini wajibu wa wazee ni kuhakikisha mambo yanakwenda vizuri.
Mzee Jumanne Gombati alisema Dodoma yenye bahati ya kuwa na vyuo
vikuu vingi, lazima wataalamu wake washiriki kufanya utafiti kwa kutumia
vyuo vyao ili ifike mahali changamoto hiyo imalizike.