Wafungwa 14 walitoroka kutoka seli za kituo cha polisi cha Ahero, Kaunti ya Kisumu.
Wengine watano walihepa Jumatano walishirikiana
kutoroka walipokuwa njiani wakisafirishwa hadi mahakama ya Eldoret
kutoka Baringo.
Kamanda wa poolisi katika Kaunti ya
Kisumu, Nelson Njiri alisema miongoni mwa waliotoroka Ahero ni washukiwa
wa mauaji na ujambazi wa kutumia mabavu.
Kwenye kisa cha Eldoret, watano hao
ambao walikuwa chini ya ulinzi wa maafisa wanne wa magereza waliokuwa
wamejihami, waligeuka ‘wanyama’ walipokaribia mji wa Kabarnet karibu
umbali wa kilomita moja hivi.
Habari zilizofikia Taifa Leo zilisema kwamba, huenda wafungwa hao walifanya njama na baadhi ya walinzi wao kabla ya kutoroka.
Akithibitisha kisa hicho kupitia kwa
njia ya simu, kamanda wa kaunti ya Baringo Bw Peter Okwanyo alisema,
wanaume hao waliwashinda na nguvu maafisa waliokuwa wakisafiri nao
walipofika katika eneo la Kiboino Hills.
Okwanyo alisema walikuwa wakienda kutoa ushahidi dhidi ya mfungwa mmoja aliyekuwa kati yao.
“Wafungwa waliotoroka walipaswa
kueleza korti ya Kabarnet yaliyojiri dhidi ya mfungwa mmoja aliyekuwa
kati yao kwenye kesi inayomkabili,” alisema Kamanda huyo.
Aliongeza, “Mmoja wao alimpiga na kumjeruhi afisa mmoja kabla ya kutoroka.”
Inasemekana wafungwa hao walikabiliwa na mashtaka ya mauaji, wizi wa mabavu na wengine wizi wa ng’ombe katika Kaunti ya Baringo.
Wadokezi kutoka gereza la Eldoret
walisema, washukiwa wote ni wa jamii ya Tugen-Kalenjin na pia waliokuwa
walinzi wao siku hiyo ni wa jamii hiyo hiyo.
Waliongeza jamaa hao walitembea kwa
ujasiri baada ya kutoroka kutoka mikononi mwa walinzi kuelekea mto Kerio
na kisha wakaonekana wakila katika kioski kimoja cha chakula katika
eneo mmoja karibu na mto huo.
“Kwa sasa hatuwezi kusema mengi
kuhusu tukio hilo ila tu uchunguzi umeanzishwa na hatua za kisheria
zitachukua mkondo wake dhidi ya maafisa wa gereza na walinzi ikiwa
itadhihirika waliwasaidia wafungwa hao kutoroka,” alisema Okwanyo.
Yamkini walienda na bunduki moja
Ripoti ambazo hazijadhibitishwa, zinasema wanaume hao walitoroka na bunduki moja ya maafisa.
Washukiwa kadhaa walinaswa Ijumaa huku wakihusishwa na sakata hiyo miongoni mwao wakiwemo waendeshaji bodaboda.
Kwingineko, mwanamume mmoja
aliyetatiza shughuli za mahakama Alhamisi mjini Eldoret na kukalia kiti
cha hakimu, Ijumaa alifunguliwa mashtaka.
Bw Robert Kipkorir Ruto alifikishwa
mbele ya hakimu mkazi Pauline Mbulikah aliposomewa mashtaka ya kuzua
vurugu na kutatiza amani huku akikabiliwa na mashtaka mengine sawia na
hayo aliyodaiwa kutekeleza mnamo Januari 28.
Alikiri mashtaka yote dhidi yake huku akisema ni kweli alishiriki uovu huo na kisha akabakia kimya asimwelewe yeyote.
“Ni kweli kuwa nilikosa kama vile kiongozi wa mashtaka anavyosema,” Ruto aliambia korti.
Kwenye mashtaka mengine, mshtakiwa
alidaiwa kuvuruga shughuli za hoteli ya Samich na kuharibia wateja
starehe katika eneo la Leleboinet, Keiyo Kusini.
Mwanamume huyo alisemekana
kuvunjavunja vioo vya madirisha na kuvitupa moja baada ya ingine huku
akilenga mwanamume mwingine kwa jina Philip Kipsang’.