Zaidi ya nyumba 200 zimezingirwa na maji katika Manispaa
ya Mtwara Mikindani kufuatia mvua zinazoendelea kunyesha na kusababisha
hasara kubwa ambayo thamani yake bado haijajulikana.
Kufuatia hali hiyo Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Halima
Dendegu ametoa saa 24 kwa wataalam kuhakikisha wanayaondoa maji ndani
ya makazi ya watu.
Mkuu wa Wilaya ya Mtwara, Wilaman Ndile amemwambia
mkuu huyo wa mkoa alipotembelea maeneo yaliyoathiriwa na mafuriko hayo
kuwa zaidi ya nyumba 200 zimezingirwa na maji katika mitaa mbalimbali ya
manispaa hiyo.
Alisema kuwa hakuna mtu aliyeripotiwa kupoteza
maisha kutokana na mafuriko hayo lakini kumetokea uharibifu mkubwa wa
mali na vyakula.
“Mvua kubwa zilizonyesha jana usiku
zimeshababisha mafuriko haya…tatizo kubwa mji wetu hauna mifereji ya
kupeleka maji baharini…athari ni kubwa sana,” alisema Ndile.
Aliongeza kuwa “Mitaa ya Magomeni, Chuno, Kiangu, Skoya,Kisutu Nabwada ndiyo yaliyoathiriwa zaidi na tatizo hili”
Alia Mussa ni mmoja wa waathirika wa mafuriko hayo
kutoka Mtaa wa Kisutu eneo la Nabwada alisema kuwa amepoteza fedha
kiasi cha Sh300,000, nguo, chakula na vyombo vya ndani.
“Tunaomba msaada kwa viongozi kunusuru hali hii,
tunaona serikali yetu kama imetutupa, hatuna chakula, wala fedha za
kununua chakula, kila kitu kimeloa,” alisema Mussa.
Dendegu amewaagiza wataalam wa mipango miji,
zimamoto na manispaa kuhakikisha ndani ya saa 24 wanayaondoa maji hayo
katika ya makazi ya watu.