Wakati macho na masikio ya Watanzania wengi yakielekea mjini Dodoma kesho katika vikao vya Bunge vinayotarajia kujadili Muswada wa Mabadiliko ya Sheria Mbalimbali, Jukwaa la Wakristo nchini limeitaka Serikali isitishe kujadili marekebisho ya Sheria ya Tamko la Sheria ya Kiislam ya mwaka 1964.
Taarifa iliyotolewa na Jukwaa hilo leo inasema
Muswada huo unaolenga kuanzishwa kwa Mahakama ya Kadhi utasabisha
kuvunjika kwa misingi ya Taifa hili kama lisilo la kibaguzi na
kufungamana na dini yeyote.
Taarifa hiyo pia ilisema mapendekezo ya
kurekebisha Sheria ya Tamko la Sheria za Kiislamu ni mapendekezo makubwa
yatakayokuwa na athari kubwa na nzito; kwani yanahoji msingi wa dola ya
Tanzania kama dola isiyokuwa ya kidini.
“Kama ambavyo tumesema mara nyingi, masuala
yanayohusu imani za dini na kujiingiza kwa Serikali katika masuala
yanayohusu imani hizo yanahitaji mjadala mpana na maridhiano ya
kitaifa,” inasema sehemu ya taarifa hiyo iliyosainiwa na Mwenyekiti wa
TEC, Askofu Dk Alex Malasusa, Mwenyekiti wa TEC, Askofu Tarcisius
Ngalalekumtwa na Mwenyekiti wa CPCT, Askofu Daniel Awet.
Kwa mujibu wa tamko hilo, Mahakama za Kadhi, pamoja na Mahakama za Wenyeji (Native Courts), zilizokuwepo wakati wa ukoloni zilifutwa na Sheria ya Mahakama za Mahakimu (Magistrates Courts Act)
ya mwaka 1963 hivyo tangu wakati huo, mahakama hizi hazipo na
hazitambuliwi na sheria yoyote. Hivyo, mapendekezo ya Muswada huu
yakipitishwa ndiyo yatazianzisha.
“Kwa mapendekezo haya, Serikali inachukua jukumu
la kuanzisha yenyewe taasisi za kidini kinyume na utaratibu wa kikatiba
ambapo Serikali imekuwa haijishughulishi na uanzishwaji na uendeshaji wa
taasisi za kidini. Hii ni kwa sababu Sheria ya Tamko la Sheria za
Kiislamu haikuanzisha mahakama au taasisi nyingine yoyote ya kusimamia
Sheria hiyo bali iliweka utaratibu wa mahakama za kawaida kuitambua na
kuisimamia Sheria hiyo.”
Tamko hilo linaeleza zaidi kuwa mapendekezo ya
Muswada huo yanaleta sintofahamu kama mamlaka za mahakama za sasa za
kusikiliza na kuamua masuala ya hadhi ya mtu, mirathi na ndoa kwa mujibu
wa Sheria ya Tamko la Sheria za Kiislamu itaendelea kuwepo.
“Aidha mapendekezo ya Muswada huu yako kimya juu
ya uhusiano wa Mahakama za Kadhi na mahakama za kawaida. Kwa mfano,
haieleweki (haikuwekwa wazi) kama kutakuwa na utaratibu wa rufaa,
marejeo na mapitio ya maamuzi ya mahakama hizo. Endapo, kwa mfano, mtu
hataridhika na maamuzi ya Mahakama ya Kadhi, je, atakuwa na haki ya
kukata rufaa? Kama atakuwa na haki hiyo, rufaa hiyo itapelekwa kwenye
mahakama au chombo gani?”
“Mapendekezo hayo hayo, pamoja na kwamba wadaawa
wataenda kwa hiari yao, yako kimya juu ya kesi zinazohusu Waislamu na
watu wa imani nyingine. Na hata kwa wadaawa ambao ni Waislamu, ikiwa
upande mmoja (tuseme wa Mdai) unakwenda kwa hiari ila upande mwingine
(wa Mdaiwa) unataka shauri lisikilizwe na mahakama ya kawaida, Muswada
hautoi jibu nini kifanyike.”
Taarifa hiyo inasema pia kuwa suala hilo la
Mahakama ya Kadhi lilikataliwa na Bunge Maalumu la Katiba wakati wa
kupitishwa kwa Katiba inayopendekezwa hivyo kushangazwa na suala hili
kuibuka kwenye Muswada huu baada ya kuwa limekataliwa.
“Sisi viongozi wa Makanisa wanachama wa Jukwaa la
Wakristo Tanzania tunaamini kwamba sababu zilizopelekea kufutwa kwa
mahakama hizi mwaka 1963; yaani, kujenga umoja wa kitaifa, kuondoa
ubaguzi katika mfumo wa kisheria na utoaji haki sawa, bado ni halali na
za msingi leo hii. Kwa sababu hiyo, kwa heshima kubwa, tunashauri
kwamba Serikali iondoe Muswada huu Bungeni ili kuepusha kuvunja misingi
ya Taifa hili kama taifa lisilo la kibaguzi na lisilo fungamana na
dini,” inasema taarifa hiyo