
CHAMA cha ACT-Tanzania kimelitaka Jeshi la Polisi nchini kuwasaka na kuwafikisha kwenye vyombo vya sheria wote waliohusika na tukio la mauaji ya aliyekuwa Mwenyekiti wa Kitongoji cha Masigo wilayani Mlele mkoani Katavi, Christian Kahongo.
Taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa jana na Katibu Mkuu wa
ACT-Tanzania, Samson Mwigamba, ilieleza kuwa chama hicho kinalaani
mauaji hayo ya kinyama ambayo hayaendani na haki za binadamu.
Alisema walimkata kichwa na kukitenganisha kabisa na kiwiliwili kisha
wakakata sehemu za siri na baadhi ya viungo vingine vya kichwa wakaanza
kuvikaanga kwenye sufuria.
Alisema huo ulikuwa ni unyama wa ajabu ambao hatujawahi kuushuhudia.
“ACT-Tanzania tumepoteza shujaa namba moja kati ya mashujaa
wanaokiwakilisha chama chetu kwenye vyombo vya Serikali. Ndiye mshindi
wa kwanza kwenye Uchaguzi wa Serikali za Mitaa kupitia ACT-Tanzania na
alipita bila kupingwa na kuwa wa kwanza kutangazwa kuwa Mwenyekiti wa
Kitongoji cha Masigo kupitia ACT-Tanzania.
“Tumepoteza shujaa kama chama taifa, Mkoa wa Katavi umepoteza shujaa,
Jimbo la Mlele wamepoteza shujaa, vivyo hivyo kwa wanachama wa Kata ya
Inyonga na tawi la Inyonga,” alisema Mwigamba.
Alisema chama kitashiriki msiba huo kwa kuwakilishwa na Mwenyekiti Taifa wa muda pamoja na Katibu wa Ngome ya Vijana Taifa.
“Ikumbukwe kuwa wauaji hawana rangi, kabila wala vyama, pia
hawachagui nani wa kumuua kama ilivyotokea hivi karibuni kwa askari wetu
katika Wilaya ya Rufiji mkoani Pwani.
“Sisi ACT-Tanzania tunalaani kwa nguvu zote mauaji haya ya kiongozi
wetu si tu kwa sababu aliyeuawa ni kiongozi wa ACT-Tanzania, bali
tutalaani na kupinga mauaji ya Mtanzania yeyote,” alisema Mwigamba.
Tukio hilo la mauaji ya kinyama lilitokea Januari 24, mwaka huu
ambapo watu wasiojulikana walivamia nyumbani kwa Christian Kahongo na
kumuua kwa kumkatakata mapanga.