VIGOGO WA CHADEMA WABURUZWA MAHAKAMANI

Jeshi la Polisi mkoani Simiyu linawashikilia wanachama tisa wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo CHADEMA wilayani Meatu wakiongozwa na Mwenyekiti wa mkoa wa chama hicho kwa madai ya kufanya vurugu na kuharibu mali.

Wanachama hao pamoja na viongozi wao mbali na kukamatwa na jeshi hilo jana, wamefikishwa mahakamani, katika Mahakama ya Wilaya ya Meatu Mkoani hapa kujibu tuhuma zinazowakabili.

Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake, Kamanda wa Polisi mkoani hapa Charlse Mkumbo, alisema kuwa wanachama hao wakiongozwa na viongozi wao walifika katika ofisi ya Mkuu wa Wilaya hiyo kusikiliza rufaa yao. Alisema kuwa chama hicho kiliwasilisha rufaa yao katika ofisi ya Mkuu wa wilaya hiyo, kupinga pingamizi lililowekwa na CCM juu ya viongozi wao waliochukua fomu kugombea nafasi mbalimbali katika uchaguzi wa Serikali za mtaa ambazo zilielezwa kujazwa kinyume cha taratibu. Mkumbo alieleza kuwa katika kesi hiyo wanachama wa chama hicho waliochukua fomu za kugombea nafasi mbalimbali walijaza neno CDM katika nafasi ya jina la chama, hali iliyopelekea CCM kupinga kwa madai kuwa hakuna chama kinachoitwa CDM. Alibainisha kuwa katika kutolewa majibu ya rufaa yao, ambayo yalikuwa yakitolewa na Katibu tawala wa Wilaya hiyo, wanachama hao wakiongozwa na viongozi wao wa Wilaya na Mkoa walikusanyika katika ofisi hiyo kusikiliza majibu hayo. Katika majibu ya rufaa yao walishindwa baada ya kuelezwa kuwa hakuna chama kinachoitwa CDM, majibu ambayo waliyapinga na kuamua kufanya vurugu ambapo walivunja kioo cha nyuma cha gari mali ya Mshauri wa mgambo wa wilaya hiyo. Alisema kuwa gari hiyo T-159 DRF ambayo ilikuwa katika eneo la ofisi hiyo, ilivunjwa kwa kurushiwa mawe na wanachama hao wakipinga maamuzi hayo, ambapo polisi waliwasili na kuwadhibiti. Mkumbo alieleza kuwa Jeshi la Polisi mkoani hapa lilifanya msako kuwatafuta waliosababisha vurugu hizo, ambapo liliwakamata Allen Mwakipesile (24) Mwenyekiti BAVICHA Meatu pamoja na Mshuda Wilson Mwenyekiti Chadema Mkoa wa Simiyu.

Wengine ni Joseph Slumu (34), Simon Wilu (39), Nghili Matula (55), Kulwa Seleman (36), Moses Chenyabu (48), Bundala Mwigulu (17) pamoja na Mwashi Tunu (23) wote wanachama wa chama hicho.

Hata hivyo Mkuu huyo wa polisi alieleza kuwa wanachama hao pamoja na viongozi wao, jana wamefikishwa mahakamani katika Mahakama ya Wilaya ya Meatu kujibu tuhuma zinazowakabili.


JIUNGE NA EDMO BLOG SASA

Usipitwe!! Jiunge nasi kupitia Facebook,Twitter na Instagram ili kupata habari zote za town! Usikose kujiunga na Youtube kuangalia video zote kali kutoka Edmo Blog Pekee!, kujiunga bonyeza hapa>>>Youtube

Tupe Maoni Yako lakini Usiandike Matusi



 
© Copyright EDMO BLOG | Designed By Peruzibongo