Mahakama ya kimataifa ya ICC imetupilia mbali kesi ya jinai inayomkabili Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta.
Mwendesha mkuu wa mashitaka Fatou Bensouda ameondoa kesi dhidi ya Kenyatta ambaye alidaiwa kutenda uhalifu dhidi ya binadamu wakati wa ghasia za baada ya uchaguzi mwaka 2007/2008.
Mahakama ilikuwa imempa Bensouda wiki moja kuamua ikiwa ataendelea na kesi dhidi ya Kenyatta au la.
Kenyatta alishtakiwa kama mshukiwa mkuu wa ghasia za baada ya uchaguzi wa 2007/2008 akituhumiwa pamoja na William Ruto ambaye ni naibu Rais kwa kutenda uhalifu dhidi ya binadamu.
Zaidi ya watu elfu moja waliuawa wakati wa ghasia hizo. Uhuru alikuwa mtu maarufu zaidi kufikishwa mahakamani na pia mshukiwa mkuu kwani alifikishwa mahakamani akiwa Rais aliye mamlakani.
Hili ni pigo kubwa kwa upande wa mashitaka, wengi walioana keshi dhidi ya Kenyatta kama mtihani mkubwa katika historia ya mahakama hio.
Upande wa mashitaka ulitaka mahakama kuupatia muda zaidi ili upate ushahidi zaidi dhidi ya Kenyatta kama vile taarifa za akaunti yake ya benki.
Upande wa utetezi uliteta kuwa ikiwa hakuna ushahidi wa kutosha kesi hiyo inapaswa kutupiliwa mbali.