RAIS Jakaya Kikwete amemwapisha rasmi Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa
Hesabu za Serikali (CAG), Profesa Mussa Juma Assad. Ameapishwa baada ya
aliyekuwepo, Ludovick Utouh, kustaafu kwa mujibu wa Sheria na Katiba.
Mara baada ya kuapishwa CAG huyo alikabidhiwa ofisi pamoja na ripoti
yenye kurasa 78 za mwongozo mzima kuhusu utendaji na changamoto za ofisi
hiyo ya Ukaguzi. Utouh ndiye aliyemkabidhi.
Sherehe za kumwapisha kiongozi huyo, zilizofanyika Ikulu Dar es
Salaam jana, zilihudhuriwa na viongozi wa Serikali, Kamati za Kudumu za
Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) na Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC)
na vyombo vya ulinzi na usalama.
Akizungumza mara baada ya kuapishwa Profesa Assad alisema
atahakikisha anatekeleza ipasavyo na kwa uaminifu majukumu ya ofisi yake
kwa kushirikiana na wenzake huku lengo kubwa likiwa ni kusimamia
matumizi na mapato ya Serikali.
“Nitatekeleza kwa uaminifu majukumu yangu yote ya ofisi ya CAG kama
yalivyoainishwa kwa mujibu wa sheria, kanuni na taratibu,” alisisitiza.
Akijibu swali la waandishi wa habari kuhusu utata uliojitokeza kwenye
ripoti ya CAG katika sakata la akaunti ya Tegeta Escow, hasa eneo
ambalo ripoti hiyo imebainisha kuwa inawezekana fedha hizo ni za umma au
la, alisema kwa sasa hawezi kuzungumzia suala hilo hadi
atakapokabidhiwa ripoti hiyo na kuisoma.
Kwa upande wake, Spika wa Bunge, Anne Makinda, alisema uteuzi huo
umekuja wakati mwafaka kutokana na ukweli kuwa kwa sasa nchi ipo katika
kipindi cha mpito baada ya sakata la Escrow, hivyo ni wakati mwafaka wa
kutengeneza sura halisi ya nchi yenye uwajibikaji na nidhamu ya fedha ya
umma.
Alisema kutokana na hali ilivyo ni vyema Ofisi ya CAG na Bunge kwa
pamoja, wakaunganisha nguvu ili kuhakikisha kunakuwa na uadilifu katika
bajeti na matumizi ya fedha za Serikali.
“Kwa kweli mtikisiko huu ni mzuri katika uendeshaji wa nchi,
unatufanya tukae sawa kwa kujenga nidhamu ya fedha, lakini pia utasaidia
kujenga muundo mzuri wa kufanya kazi, ili nchi isimame vizuri ni lazima
ipite kwenye hali iliyopo sasa,” alisema Makinda.
Waziri wa Fedha, Saada Salum Mkuya, alisema Wizara yake ina matarajio
makubwa baada ya uteuzi huo wa CAG na itahakikisha inafanyakazi na
ofisi hiyo kwa ushirikiano kwa manufaa ya Watanzania.
Akijibu swali kuhusu mwenendo wa maadili ya viongozi, hasa kutokana
na sakata lililotikisa nchi la akaunti ya Escrow, Mkuya alisema wizara
yake inaendelea kuchukua hatua mbalimbali ili kuhakikisha taratibu,
kanuni na sheria za fedha zinafuatwa.
“Maadili tunapambana nayo, wizara itahakikisha taratibu na sheria za
fedha zinafuatwa, lakini pia tutaendelea kuwachukulia hatua wale wote
wanaoenda kinyume na taratibu na sheria zilizopo, nawahakikishia suala
hili tunalichukulia kwa mapana,” alisema.
Utouh alisema uteuzi huo umekuja wakati mwafaka kutokana na ukweli
kuwa ofisi hiyo ni nyeti na si vizuri kukaa muda mrefu ikiwa haina CAG
kamili, hali inayoweza kusababisha isiwe na nguvu.
Alisema tangu astaafu Septemba 19, mwaka huu, imepita miezi minne
ofisi hiyo ikiongozwa na Kaimu CAG. “Nimewaachia ofisi iliyo madhubuti,
imara na yenye wachapakazi, natumaini mazuri yote yataendelezwa kwa
manufaa ya Taifa letu,” alisema.
CREDITS KWA HABARILEO