Bw Nicholas Chege Mwangi, dereva wa basi nambari KBT 903R la Githurai 44, akiwa kortini Novemba 28, 2014. Picha/PAUL WAWERU
SERIKALI imesimamisha leseni ya kampuni ya matatu ya Nazigi Sacco kwa muda wa wiki mbili, baada ya wahudumu wake kushtakiwa kwa kumvua mwanamke nguo katika Barabara ya Thika.
Mkurugenzi wa Mamlaka ya Kitaifa ya
Uchukuzi (NTSA) Francis Meja aliipa kampuni hiyo wiki mbili kuwasilisha
magari yao yote 243 kwa ukaguzi. Sacco hiyo ina magari takriban 243.
Kamanda wa Trafiki Charlton Mureithi
pia atahakikisha kuwa hakuna gari lolote la kampuni hiyo ambalo
litahudumu hadi suala hilo litatuliwe.
Serikali pia inachunguza matatu
ambazo zilihusika katika visa vingine viwili katika majuma mawili
yaliyopita katika eneo la Kayole na barabara ya Tom Mboya.
Dereva na makanga wa basi moja la
sacco hiyo ambapo abiria mmoja mwanamke alivuliwa nguo na kudhulumiwa
kimapenzi kwa saa kadha wataendelea kuzuiliwa kwa siku 21 zijazo, huku
polisi wakiendelea na uchunguzi wao.
Bw Nicholas Chege Mwangi na Bw
Meshack Mburu Mwangi, ambao ni dereva na utingo wa basi hilo, lenye
nambari za usajili KBT 903R wanazuiliwa katika kituo cha polisi cha
Kasarani na wanatarajiwa kuwafichua wahusika, ambao wanasemekana
kutoroka.
Mahakama Nairobi iliambiwa kuwa
polisi walikuwa wakichunguza visa mbalimbali vya dhuluma za kimapenzi,
na wameanzisha uchunguzi dhidi ya visa kadha vya dhuluma za kimapenzi na
kuvuliwa nguo kwa wanawake jijini Nairobi, ili kuwakamata na kuwashtaki
wahusika.
Upande wa mashtaka pia uliwaomba
waathiriwa wa dhuluma hizo, ambao hawajajitokeza baada ya kushambuliwa
katika maeneo hayo mawili kujitokeza ili kuandikisha taarifa kwani
washukiwa hao tayari washakamatwa.
Kuzua hofu
“Kumekuwa na ongezeko la kuvuliwa
nguo kwa wanawake pamoja na dhuluma za kimapenzi, hali ambayo imezua
hofu miongoni mwa umma. Uchunguzi tuliofanya ulipelekea kukamatwa kwa
washukiuwa mnamo Novemba 27 katika Barabara ya Thika,” akasema Duncan
Ondimu, ambaye ni kiongozi wa mashtaka katika wasilisho lake kwa
mahakama.
Katika kesi tofauti, polisi mmoja wa
utawala na abiria mmoja wa kiume wamefikishwa mahakamani kwa kujaribu
kumvua nguo msichana mmoja, aliye mwanafunzi mmoja wa shule katika basi
moja.
Watu watano pia wameshtakiwa kwa
kuwatoa wanawake nguo katika mtaa wa Kayole. Kisa hicho, ambacho
kilifanyika katika mtaa wa Kayole kingali kinachunguzwa. Tukio la
barabara ya Tom Mboya pia lingali kinachunguzwa.
Jana, upande wa mashtaka ulisema
kuwa waliwahoji washukiwa hao wawili lakini “hawakuwa bado wamewafichua
washukiwa waliohusika katika kitendo hicho” lakini walikuwa wakifuata
habari muhimu zitakazopelekea kukamatwa kwao.
Kiongozi huyo wa mashtaka alisema kuwa mhusika katika kisa cha basi la Githurai 44 bado hajatambuliwa.