WAKAZI
40 wa Tarafa ya Inyonga, Makao Makuu ya Wilaya ya Mlele mkoani Katavi
wamekamatwa baada ya kukutwa wakinywa pombe asubuhi vilabuni na kwenye
maduka yanayouza aina mbalimbali ya vinywaji.
Wakazi
hao ni pamoja na wanywaji wenyewe na wauzaji wa pombe hizo wakiwemo pia
wachezaji wa mchezo wa pool ambapo walikiuka amri ya Mkuu wa Wilaya,
Kanali Ngelela Lubinga ya kutocheza pool au kunywa pombe hadi baada ya
saa za kazi za ujenzi wa taifa, yaani kuanzia saa 10 jioni.
Hivi
karibuni, Kanali Lubinga aliamuru wakamatwe baada ya kubainika kukiuka
amri yake inayowakataza watu kunywa pombe wala kucheza mchezo wa pool
asubuhi.
Aliamuru
wanamgambo wanaofanya mafunzo wawasake na kuwakamata watu hao na
aliiamuru waadhibiwe kwa kuchimba vyoo, kuzibua mitaro na mashimbo ya
kutupia taka katika mji huo wa Inyonga kwa siku tatu mfululizo.
Kwa
mujibu wa Kanali Lubinga operesheni hiyo ni endelevu na yeyote
atakayekamatwa akikiuka amri yake hiyo adhabu yake ni kufanya usafi wa
mji mzima wa Inyonga.
“Tabia
hii ya unywaji wa pombe na kucheza pool asubuhi haikubaliki kabisa,
lazima watu wajenge tabia ya kujituma kufanya shughuli zao za maendeleo
badala ya kuendekeza kunywa pombe na starehe asubuhi,’’ alisisitiza.