Serikali
mkoani kilimanjaro imewaondoa hofu wananchi kwa kupinga taarifa za
uwepo wa ugonjwa wa Ebola ambao umekuwa tishio kwa nchi za aArika
kufuatia taarifa za kugundulika kwa mgonjwa mwenye Dalili za ugonjwa huo
katika kituo cha afya Shirimatunda manispaa ya Moshi.
Mkuu wa mkoa wa Kilimanjaro Bw. Leonidas Gama amesema mgonjwa huyo
amepelekwa katika kituo hicho kilichotengwa kwa ajili ya wagonjwa
watakaogundulika kuwa na viashiria vya ugonjwa huo kutokana na histori
ya mgonjwa huyo ambaye alikuwa na homa kali kuonyesha alikuwa ametokea
nchini Senegal.
Amesema mgonjwa huyo kwa sasa anaendelea vizuri na kwamba vipimo
vya awali vimeonyesha mgonjwa huyo alikuwa na ugonjwa wa maleria na
kwamba tayari ameshatolewa sampuli na kupelekwa jijini Dar es salaamu
kwa ajili ya uchunguzi zaidi.
Kwa upande wake mganga mkuu wa mkoa wa kilimanjaro Dk Mtumwa Mwako
amewataka wananchi kuchukua tahadhari za kukabiliana na ugonjwa huo kwa
kuepuka salamu za kushikana mikono.
Nao baadhi ya wananchi wa manispaa ya moshi wameiomba serikali
kutoa elimu zaidi kwa wananchi juu ya ugonjwa huo na kuchukua tahadhari
za kukabiliana na wageni wanaoingia hapa nchini.