Na Mwandishi Wetu
RAIS
wa awamu ya tatu wa Tanzania, Benjamin Mkapa amewaongoza maelfu ya
waombolezaji katika mazishi ya aliyekuwa Meja Jenerali Herman Corneli
Lupogo kwenye makaburi ya Kinondoni jijini Dar es Salaam.
Viongozi wengine walioudhulia mazishi hayo ni, Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dk. Hussein
Mwinyi,
Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi, Jenerali Davis Mwamunyange, Jenerali Mstaafu
Robert Mboma pamoja na Mawaziri waliowai kuongoza Wizara ya Ulinzi na
Jeshi la Kujenga, Prof, Philemoni Sarungi na Edgar Maokola Majogo.
Akisoma
risala mara baada ya mazishi, Mwakilishi wa Jeshi, Meja Jenerali Gaudence Milanzi alisema,
marehemu alifariki dunia mnamo Oktoba 19, mwaka huu kwa ugonjwa katika
Hospitali Kuu ya Jeshi Lugalo alikokuwa akipata matibabu.
Alisema,
marehemu alimaliza elimu ya Kidato cha sita katika shule ya Sekondari Pugu
mwaka 1956, baadae akapata Stashahada ya Ualimu na Shahada ya kwanza ya Sanaa
katika Chuo Kikuu cha Makerere nchini Uganda.
“Marehemu
alijiunga na Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania mnamo Julai 23, 1965 na
kutunukiwa Kamisheni Januari 21, 1966 na baadae kwa nyakati tofauti
alipandishwa vyeo hadi kufikia Cheo cha Meja Jenerali mnamo Februari 9, 1983
ambacho alistaafu nacho Jeshini,”alisema.
Aliongeza
kuwa, baada ya marehemu kustaafu aliendelea na shughuli mbalimbali za kujenga
taifa ikiwamo, kuwa Mkuu wa Mkoa Iringa mwaka 1990, Mwenyekiti Chuo cha
Diplomasia 1987 hadi 1991, Mkurugenzi Mtendaji wa AICC 1993.
“Pia
alikuwa Mwenyekiti wa Tume ya Kudhibiti Ukimwi Tanzania(TACAIDS), 2001 hadi
2014, marehemu mara kwa mara alienda kushiriki kutoa mihadhara kama mwalimu wa
kualikwa katika Vyuo mbalimbali vya ndani na nje ya Jeshi ikiwamo Chuo cha
Taifa cha Ulinzi (NDC),”alisema.
Aidha,
alimalizia kwa kutoa salamu za rambirambi kwa niaba ya Maafisa, Askari na
Watumishi wa Umma wa JWTZ kutokana na msiba mzito uliotokea na kwamba sio pigo
kwa familia yake, bali kwa ndugu, jamaa, majirani, jeshi na Taifa kwa ujumla.
Rais
mstaafu wa awamu ya tatu, Benjamin Mkapa na mkewe wakiweka shada la
maua katika kaburi la Meja Jenerali mstaafu, Herman Lupogo wakati wa
mazishi yake katika makaburi ya Kinondoni jijini Dar es Salaam. Meja
Lupogo alifariki Oktoba 19 katika hospitali ya Jeshi ya Lugalo.
Mke wa marehemu akiweka shada la maua.
Familia ikiweka shada la maua.
Mkuu wa Majeshi Jenerali Davis Mwamunyange akiweka shada la maua.
Mashada ya maua yakiwekwa.
Heshima kwa marehemu Meja Jenerali Herman Lupogo.