RAIS
Jakaya Kikwete amesema mfumo unaotumika Tanzania ambako Rais anatumikia
nafasi ya uongozi kwa muhula wa miaka mitano na si zaidi ya miaka 10 ni
mzuri na unaovutia kwa sababu unaiwezesha nchi kupata fikra na mawazo
mapya.
Aidha,
Rais Kikwete amesema, anaamini Tanzania itapata Rais bora zaidi kuliko
yeye, atayeiwezesha Tanzania kusonga mbele kwa kasi kubwa zaidi.
Rais
Kikwete pia amesema, ana hamu kumaliza muda wake wa uongozi ili arudi
kijijini kushughulika na wajukuu wake na mifugo yake. Rais Kikwete
ametoa kauli hiyo mjini Beijing, China, wakati akizungumza na mabalozi
wa Afrika wanaoziwakilisha nchi zao katika China.
Mkutano
huo uliofanyika kwenye Nyumba ya Kufikia Wageni wa Serikali ya China ya
Diaoyutai, ulikuwa shughuli ya kwanza ya Rais Kikwete katika ziara yake
rasmi ya siku sita ya Jamhuri ya Watu wa China ambako amealikwa na Rais
Xi Jinping.
Wakati
wa maswali na majibu, Balozi Sola Onadipe, Naibu Balozi wa Nigeria
katika China, alishangazwa na kauli ya Rais Kikwete kuwa anatamani
amalize muda wake wa uongozi ili astaafu na kusema kuwa lingekuwa jambo
la maana kwa Afrika kama viongozi wengine wangekuwa na mawazo ya namna
hiyo ya kuheshimu Katiba za nchi zao na kung’atuka kwenye uongozi muda
wao unapowadia.
Rais Kikwete amemwambia Balozi huyo:” Ni
kweli naona kama muda hauendi kwa kasi ya kutosha ili niweze kuwa raia
wa kawaida na nipate muda wa kuchunga ng’ombe na mbuzi wangu na nilime
mananasi yangu kwa nafasi ya kutosha. Lakini Mheshimiwa Balozi
usishangazwe na utayari wangu kuondoka katika uongozi.”
“Kwanza
utaratibu huu wa miaka mitano ama miaka 10 ni utaratibu wa Kikatiba, ni
jambo lililoko katika Katiba yetu na hatuna kishawishi cha
kulibadilisha. Pili, kazi hii ya Urais ni kazi ngumu sana. Kwa hakika,
binafsi nawaonea gele sana wenye nguvu na ubavu wa kutaka kubakia kwenye
kazi hii kwa miaka mingi. Pengine wana nguvu zaidi kuliko mimi,” amesema Rais Kikwete na kuongeza:
“
Lakini pia kuna uzuri katika mfumo huu wa kwetu kwa sababu kila baada
ya miaka mitano na hata kama ni baada ya kila miaka kumi, anaingia mtu
mwingine madarakani akiwa na fikra mpya na mawazo mapya.”
“Mfumo
huu ni mfumo unaoniridhisha sana na wala hakuna kinachonishawishi
nibakie katika madaraka zaidi ya muda wangu kikatiba. Nina hakika, nchi
yetu itapata kiongozi mwingine, bora kuliko hata mimi, kuongoza vizuri
nchi yetu.”
Rais
Kikwete pia amesema kuwa si busara pia kwa kiongozi kuwasikiliza wale
wanaoshauri wakisema kuwa akiondoka madarakani nchi itavurugika.
“Kwa
hakika, hawa wanatetea maslahi yao tu wakisema kuwa ukiondoka wewe
madarakani, wao hawatakuwa tena mabalozi ama mawaziri ama nafasi
nyingine yoyote.”