Baadhi
ya washiriki wa Semina ya Usambazaji wa Matokeo ya Sensa ya Watu na
Makazi ya Mwaka 2012 wakifuatilia masuala mbalimbali leo mkoani Pwani.
Kamishna
wa Sensa ya Watu na Makazi 2012 Hajjat Amina Said Mrisho akimkabidhi
machapisho ya Sensa Mkuu wa Mkoa wa Pwani Bi. Mwantumu Mahiza akizindua rasmi Usambazaji wa Matokeo ya Sensa ya Watu na Makazi ya
Mwaka 2012 leo mkoani Pwani.
Mkuu
wa Mkoa wa Pwani Bi. Mwantumu Mahiza (aliyekaa) akizindua rasmi
Usambazaji wa Matokeo ya Sensa ya Watu na Makazi ya Mwaka 2012 leo
mkoani Pwani. Nyuma yake ni viongozi wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu
wakiongozwa na Mkurugenzi Mkuu Dkt. Albina Chuwa (kushoto).
Baadhi
ya washiriki wa Semina ya Usambazaji wa Matokeo ya Sensa ya Watu na
Makazi ya Mwaka 2012 wakiangalia moja ya ramani inayoonyesha takwimu
ya Mgawanyo wa Watu kwa umri na Jinsi na taarifa za Msingi za
Kidemografia, Kijamii na Kiuchumi.
Washiriki
wa Semina ya Usambazaji wa Matokeo ya Sensa ya Watu na Makazi ya Mwaka
2012 wakiangalia moja ya ramani inayoonyesha takwimu ya Mgawanyo wa
Watu kwa umri na Jinsi na taarifa za Msingi za Kidemografia, Kijamii na
Kiuchumi.
Washiriki wa Semina ya Usambazaji wa Matokeo ya Sensa ya Watu na Makazi ya Mwaka 2012 wakiwa katika picha ya pamoja.
Picha na Habari na
Aron Msigwa–MAELEZO
Ofisi
ya Taifa ya Takwimu imezindua rasmi usambazaji wa matokeo ya Sensa ya
Watu na Makazi ya mwaka 2012 na kuwataka wadau mbalimbali wakiwemo
viongozi wa wilaya na mikoa kote nchini kuanza kutumia na kuhamasisha
matumizi ya takwimu rasmi zilizotolewa na ofisi hiyo katika kupanga
mipango ya maendeleo.
Hayo
yamebainishwa leo mkoani Pwani na Mkurugenzi Mkuu wa Ofisi ya Taifa ya
Takwimu Dkt. Albina Chuwa wakati akiwakaribisha viongozi, watendaji na
wadau mbalimbali wa mkoa wa Pwani waliohudhuria semina ya usambazaji wa
Matokeo ya Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2012.
Amesema
Tanzania ina takwimu bora kutokana na kazi kubwa iliyofanywa na Ofisi
yake kwa kushirikiana na Ofisi ya Mtakwimu Mkuu wa Serikali ya Mapinduzi
ya Zanzibar kuandaa na kukamilisha taarifa za matokeo ya Sensa
yakiwemo machapisho matatu yanayohusu Idadi ya Watu katika ngazi ya
Utawala, chapisho la Mgawanyo wa Watu kwa umri na Jinsi na chapisho la
Taarifa za Msingi za Kidemografia, Kijamii na Kiuchumi.
Dkt.
Chuwa ameeleza kuwa Ofisi ya Taifa ya Takwimu inaendelea na mikakati
mbalimbali ya kuhamasisha matumizi ya takwimu za matokeo ya Sensa katika
ngazi ya mkoa, wilaya na vijiji ili ziweze kutumika katika kupanga
mipango ya maendeleo.
Ameeleza
kuwa takwimu zitakazowasilishwa katika maeneo mbalimbali katinga ngazi
ya kijiji, wilaya na mikoa ukiwemo mkoa wa Pwani ambao umezindua rasmi
shughuli hiyo ya usambazaji wa matokeo zitahusu Umri, Jinsi na Viashiria
muhimu vya umri katika makundi, hali ya ndoa, hali ya uyatima na vifaa
vilivyotumika katika ujenzi wa nyumba .
Amesema
lengo la usambazaji wa takwimu hizo ni kueleza hali halisi ya mafanikio
ya mikoa katika Nyanja za uchumi, umasikini, elimu na afya ili
kuwezesha uboreshaji wa maeneo ambayo hayafanyi vizuri.
Kwa
upande wake Mkuu wa Mkoa wa Pwani Bi. Mwantumu Mahiza akizindua rasmi
Usambazaji wa Matokeo ya Sensa ya Watu na Makazi ya Mwaka 2012 kwa ngazi
ya vijiji, Wilaya na mikoa ameeleza kuwa usambazaji wa matokeo
hayo utawasaidia na kuwarahisishia viongozi wa maeneo mbalimbali
kupanga Bajeti na mipango ya maendeleo.
Amesema
matumizi ya takwimu sahihi yatawezesha upelekaji wa huduma za jamii
zikiwemo shule, hospitali, ujenzi wa masoko, huduma za maji na
kuirahisishia serikali kuwafikishia wananchi huduma hizo kutokana na
takwimu zilizoainishwa katika maeneo husika na kuiepusha serikali
kuwekeza fedha nyingi katika miradi ambayo haiendani na idadi ya watu
katika eneo husika.
Ameongeza
kuwa matumizi ya takwimu hizo kuanzia ngazi ya familia hadi taifa
yatasaidia kupunguza na kuondoa migogoro ya ardhi hususani kurahisisha
suala la umiliki na mgawanyo wa ardhi kulingana na idadi ya watu na
huduma.
Bi.Mahiza
ametoa wito kwa viongozi mbalimbali wa serikali na madhehebu ya dini
kote nchini kuwahamasisha wananchi kutumia takwimu zitakazosambazwa
katika maeneo mbalimbali nchini.
Naye
mwakilishi wa Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia idadi ya
watu Duniani (UNFPA) nchini Tanzania Bw.Colins Opiyo akizungumza wakati
wa ufunguzi wa semina hiyo amesema kuwa UNFPA itaendelea kushirikiana na
Tanzania ili kuhakikisha kuwa Tanzania inakuwa na takwimu sahihi.
Amesema
kuwa ili takwimu ziwe sahihi lazima ziendane na uhalisia wa eneo
husika, zitolewe katika muda maalum , zikidhi vigezo vilivyowekwa
kimataifa na kutafsiriwa kulingana na shughuli za kiuchumi za wananchi
wa Tanzania wakiwemo wakulima, wafugaji na wafanyabiashara.