KAMATI ya Maudhui ya Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), imetoa onyo kali kwa kituo cha Redio cha Times Fm, pamoja na faini ya kulipa kiasi cha Sh milioni 1, kutokana na kukiuka vifungu vya maadili na kanuni za utangazaji, vilivyopo katika leseni ya utangazaji inayotolewa na mamlaka hiyo.
Akisoma
hukumu hiyo jijini Dar es Salaam jana, Mwenyekiti wa kamati hiyo,
Margareth Munyagi, alisema ‘ Times Fm’ imepewa adhabu hiyo baada ya
watangazaji wake kukiuka taratibu zilizowekwa na mamlaka hiyo, kwa
kutangaza hewani maneno yanayokiuka maadili ya utangazaji.
Munyagi
alisema kwa nyakati tofauti kupitia kipindi chake cha ‘Hatua tatu’
kilichorushwa saa 3 hadi saa 5 asubuhi na ‘Mitikisiko ya Pwani’,
kilichorushwa mchana wa Agosti 29 mwaka huu, watangazaji wa vipindi
hivyo walisikika wakizungumzia dondoo zilizolenga kuhamasisha ngono bila
kuzingatia muda huo ambao watoto wengi wanaweza kusikiliza.
Alisema
kiutaratibu muda ambao dondoo hizo zilikuwa zikitangazwa, si muda
muafaka kwa kuwa vipindi hivyo pia vingewezwa kusikilizwa na watoto na
kwamba muda wa dondoo kama hizo kutolewa unapaswa kuanzia saa 3 usiku
hadi saa 11 alfajiri.
Aidha
alisema utetezi uliotolewa na Mkurugenzi wa Redio hiyo, Leule Nyaulawa
haukidhi haja mbali na kulipokea shitaka lililotolewa dhidi yao.
Nyaulawa
alisema suala la kupata watangazaji wazuri Tanzania bado ni changamoto
kutokana na vyuo vingi kuzalisha watangazaji wasio na uwezo mzuri.
Pia
alisema kupitia kwa utetezi wake watakwenda kulifanyia kazi suala hilo
ili kuepusha kurudiwa kwa kosa kama hilo na mengine yaliyopo katika
leseni za utangazaji huku kamati hiyo ikitoa muda wa mwezi mmoja kwa
Times Fm kulipa faini hiyo au kukata rufaa kama haikuridhika na uamuzi
uliotolewa dhidi yao.