Mwili wa marehemu huyo aliyefariki dunia Septemba
4, mwaka huu umehifadhiwa katika Hospitali ya Rufaa ya KCMC na umekuwa
ukilipiwa Sh9,000 kwa siku, hivyo siku 34 gharama yake imefikia
Sh306,000.
Tukio hilo limekuwa gumzo mjini Moshi hasa baada
ya kutokea siku chache baada ya maiti nyingine ya Steven Assey
kufukuliwa kwa amri ya Mahakama na hadi leo ni siku ya 29 bado
haijazikwa licha ya mke mdogo wa marehemu, Fortunata Lyimo kupewa haki
ya kuzika lakini amekataa akisema ni kinyume cha mila na utamaduni wao
kwa mtu kuzikwa mara mbili.
Akizungumza jana, mama mzazi wa Rosemary
Marandu, Felicia Nkya, alidai kuwa mumewe aitwaye Flavian Marandu ndiye
anayeshikilia mwili huo hadi leo.
Marandu ni Diwani wa Kata ya Mrao Keryo kwa tiketi
ya CCM na anamiliki vitega uchumi kadhaa vikiwamo viwanda vya kupasua
mbao na nyumba za kulala wageni.
“Ukweli ni kwamba tangu amekufa (Marandu) hajatupa
taarifa yoyote zaidi ya kunitumia meseji ya simu akiniuliza kama mume
wa Rosemary ameniambia kama Rosemary amekufa. Kwa mila na utamaduni
wetu, mtu akifa tunakaa pamoja na kupanga mazishi lakini hadi leo
hajatuma mtu yeyote kuzungumza na sisi juu ya msiba.”
Felicia alisema walitengana na mumewe huyo mwaka
1982 na mtoto wao huyo amezaa watoto wanane na wanaume tofautitofauti na
mumewe aliyemfia, Sigfrid Mlingi naye amezuiwa kumzika.
“Naumia sana napata mateso makubwa ya kiakili na
kisaikolojia. Mwezi mzima sasa sijui hatima ya mazishi ya mtoto wangu.
Hakuna chakula kinachopita naomba mnisaidie jamani,” alilalamika.
Mama huyo alidai kuwa awali walikwenda kulalamika
polisi ambako walishauriwa kufungua shauri mahakamani lakini akadai
kwamba hawana nguvu ya kushindana na Marandu.
“Tumeamua kumkabidhi Mungu kwa sababu hatuwezi
kushindana naye (Marandu) tukamshinda. Hata kule KCMC anadai kuna kesi
mahakamani lakini sisi hatujafungua kesi,” alidai.
Mumewe azungumza
Mlingi alisema ameamua kujiweka kando kushughulikia mazishi ya mkewe baada ya baba mkwe kumtolea lugha isiyofaa.
“Mimi ndiye nilimuuguza hapo Mawenzi mpaka
akanifia mikononi mwangu na baada ya kufa nilikwenda Keryo na kuonana na
baba yake lakini akanifukuza,” alidai Mlingi.