VERONICA ROMWALD NA MICHAEL SARUNGI, DAR ES SALAAM
RAIS mstaafu wa awamu ya pili wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar,
Abood Jumbe Mwinyi (94), yupo hoi baada ya kulazwa katika Hospitali ya
Taifa Muhimbili akisumbuliwa na maradhi ya moyo.
Akizungumza jana, Ofisa Uhusiano wa
Hospitali ya Muhimbili, Doris Ishenga, alisema Jumbe alipokewa
hospitalini hapo tangu Oktoba 12, mwaka huu.
Amelazwa katika Taasisi ya Moyo baada ya kufanyiwa uchunguzi wa kina.
Alisema kwa mujibu wa taarifa za madaktari za Kitengo cha Moyo
hospitalini hapo, baada ya kumfanyia uchunguzi wamebaini Jumbe
anasumbuliwa na ugonjwa wa moyo hali inayobabishwa na kuwa na umri
mkubwa.
“Ni kweli Alhaj Jumbe alifikishwa hapa Muhimbili tangu Jumamosi
iliyopita na amelazwa katika wodi ya moyo akisumbuliwa na maradhi ya
moyo.
“Unajua ugonjwa huu unawapata zaidi watu wenye umri mkubwa, madaktari
wamesema hali yake si mbaya na wala si nzuri sana,” alisema.
Jumbe alikuwa Rais wa Zanzibar kuanzia mwaka 1972 hadi 1984 akishika
nafasi hiyo baada ya kuuawa kwa aliyekuwa Rais wa Kwanza wa Zanzibar,
marehemu Abeid Aman Karume Septemba 5, 1972.
Alijiuzulu mwaka 1984 baada ya kutokea mfarakano wa kisiasa kati yake
na viongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), kutokana na kile
kinachoelezwa kuwa na msimamo wa kutaka mfumo wa Serikali tatu ili
Zanzibar iwe na mamlaka yake kamili.
Baada ya kutoa msimamo huo, Jumbe alipata upinzani ndani ya Serikali na chama chake na kutakiwa ajiuzulu urais wa Zanzibar.
Baada ya uamuzi kutolewa kwenye vikao vya juu vya CCM, Jumbe aliachia
nafasi hiyo ambayo ilichukuliwa na Ali Hassan Mwinyi mwaka 1984, ambaye
baada ya mwaka mmoja alichaguliwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano.