AFISA wa polisi alijeruhiwa vibaya na
wenzake 7 wakatoroka waliposhambuliwa wakisindikiza gari lililobeba
karatasi za mtihani wa KCSE katika Kaunti ya Turkana.
Maafisa hao 8
walikuwa wakisindikiza gari hilo kupeleka karatasi za mtihani shule ya
mseto ya Kapendo waliposhambuliwa na watu wasiojulikana.
Baada ya
maafisa hao kutoroka, wavamizi waliteketeza gari hilo. Kulingana na
mwakilishi wa wanawake wa kaunti ya Turkana Bi Joyce Emanikor, gari hilo
lilishambuliwa eneo la Kasarani kati ya vituo vya biashara vya Lomelo
na Kapedo.
“Hatukuamini
tulipopokea habari hizo tukisherehekea sikukuu ya Mashujaa Dei katika
Lokori. Tulipata habari hizo muda mfupi kabla ya mkuu wa wilaya kusoma
hotuba ya Rais Uhuru Kenyatta,” akasema Bi Emanikor.
Aliongeza
kuwa kuna hali ya taharuki katika eneo hilo lililo karibu na mpaka wa
Kaunti ya Baringo akisema matokeo yatakuwa mabaya kwa sababu ya ukosefu
wa usalama eneo hilo.
“Wanakijiji
wanalazimika kukaa ndani ya nyumba. Kila gari linashambuliwa na shughuli
zimeathirika na uhaba wa chakula unatarajiwa eneo hili,” akasema.
Kisa hicho
kinajiri siku moja baada ya shule nne karibu na mpaka huo kufungwa kwa
muda usiojulikana kufuatia mashambulizi ya mara kwa mara.
Mwalimu mkuu
wa shule ya msingi ya Kapedo Bw Joseph Emoit Ekorukou kwa wakati huu
amelazwa katika hospitali ya St Lukes mjini Eldoret baada ya kujeruhiwa
kwenye shambulizi Ijumaa iliyopita. Shambulio hilo lilifanya walimu
kulalamika.
Walimu Kususia kazi
29 wa shule
ya upili mseto ya Kapedo, shule ya msingi ya wasichana ya Kapedo,
shule ya msingi ya Lomelo na shule ya msingi ya mseto ya Kapedo
waliamua kususia kazi hadi hali ya usalama irejeshwe eneo hilo.
Watahiniwa
wote 25 kwa sasa wamewekwa chini ya ulinzi mkali wa maafisa wa GSU.
Mkurugenzi wa Elimu wa kaunti hiyo Dkt Nichodemus Anyang aliwasiliana
na Baraza la Mitihani nchini na kusema wanajadili uwezekano wa kutuma
karatasi kwa ndege au kuhamishia watahiniwa eneo salama huko Lokori.
Mwalimu Mkuu wa shule hiyo Daniel Namunwa alisema watahiniwa hao wameshtusha na tukio hilo.