Uchaguzi
huru na wa haki utafanikiwa iwapo wananchi watapewa elimu sahihi ya
uraia na upigaji kura itakayohamasisha wapiga kura kufanya maamuzi
sahihi wakati wa uchaguzi.
Hayo yamesemwa na Kamishna wa Tume ya Taifa
ya Uchaguzi (NEC) Jaji John Mkwawa kwenye washa ya siku nne ya wadau wa
utekelezaji wa mradi wa uchaguzi unaolenga kuboresha demokrasia na amani
nchini kuelekea uchaguzi mkuu ujao .
Kamishina
alisema elimu ya uraia ni muhimu kwa wananchi ili kuwahamasisha
ushiriki wao katika demokrasia na kwamba haipaswi kuwa na utashi wa
kisiasa au upendeleo kwa chama chochote cha siasa.
Akitoa
mada katika warsha hiyo inayofadhiliwa na shirika la Umoja wa Mataifa
linaloshughulikia maendeleo (UNDP) Jaji Mkwawa alisema katika kutoa
elimu hiyo wanahabari hawana budi pia kuzingatia miongozo iliyowekwa ya
kutofungamana upande wowote kisiasa na kutoa habari kwa usahihi
kuhakikisha kwamba makundi yote yanapewa fursa na haki sawa.
“Pamoja
na changamoto zinazozikabili redio jamii, zina mchango mkubwa katika
mchakato wa uchaguzi kwa sababu idadi kubwa ya Watanzania hawajui kusoma
na kuandika hivyo kutegemea redio. Kwa misingi hiyo ni vyema kwa
waandishi wa habari wa redio jamii kusaini mwongozo wa maadili ambayo
yataonyesha utekelezaji wao kwa kutopendelea chama chochote cha siasa au
mgombea yoyote yule ”.
Amependekeza
pia umuhimu wa kuielewa jamii inayolengwa wakati wa kutayarisha vipindi
vya elimu ya uraia na utekelezaji ili taarifa zinazotolewa kwao
zikidhi matakwa ya sehemu hiyo. Kamishna wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi
Jaji John Mkwawa ametoa mfano wa kuilewa jamii kuwa ni pamoja na
kufahamu sababu zinazowafanya wananchi wasijitokeze kwa wingi katika
upigaji kura iwapo kunasababishwa na ukosefu wa taarifa muhimu na
sahihi, kukosa motisha ya kupiga kura, utashi na kutokuwepo kwa
ushindani katika kugombea.
“Katika
uchaguzi mkuu mwaka 2010 watu wachache sana walijitokeza kupiga kura
pamoja na jitihada zote za kuhamasisha na kuelimisha upigaji kura, na
baadhi ya sababu ni kwamba kupiga kura hakutampa faida yoyote mpiga
kura, au kupiga kura hakutaleta mabadiliko yoyote na kutouamini mfumo
mzima wa uchaguzi”.
Masuala
mengine yanayopaswa kufahamika ni sehemu wanakoishi walengwa ili
kubaini iwapo kuna miundombinu ya kutosha hususan kiwango cha elimu na
uelewa wao katika masuala ya uchaguzi ili kurahisisha utekelezaji wa
mradi husika.
Amezishauri
redio za jamii pia kuelewa ni mabadiliko gani yametokea katika uongozi
wa uchaguzi, kanuni na maelekezo ya uchaguzi na sababu mbalimbali
zinazotakiwa kuwafahamisha walengwa wa makundi mbalimbali wakiwemo
wanawake, watu wenye ulemavu, vijana na makundi maalum hususan wazawa,
wachungaji, watu wanaoishi na Virusi vya Ukimwi na Watu wenye ulemavu wa
ngozi ili waweze kushiriki kikamilifu katika uchaguzi.
Wakati
huo huo Godfrey Mulisa akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mkazi wa
UNDP Philippe Poinsot alikumbusha baadhi ya masuala muhimu yanayotakiwa
kufanyinywa na redio za jamii katika kipindi hiki kuelekea uchaguzi mkuu
mwaka 2015.
Ameyataja
masuala hayo kuwa ni kuibua mapema maovu mbalimbali yanayohusiana na
uchaguzi yanayoweza kujitokea ili yarekebishwe mapema, ukiukwaji wowote
wa upigaji kura utakaoenda kinyume cha sheria, kuhamasisha watu wenye
sifa za kupiga kura wajitokeze kwa wingi na kutoa ulingo kwa vyama vya
siasa kuelezea sera za vyama vyao vya siasa kwa wapiga kura wao.
Mambo
mengine ni kuibua matukio yanayohatarisha amani na utulivu, kuwaelezea
wapiga kura kwa ufasaha na lugha rahisi sheria za uchaguzi, kuwaeleza
wananchi umuhimu wa kupiga kura na masuala muhimu yanayowahusu hususan
wazee, wanawake, maskini na wasiofikiwa kwa urahisi.
Mulisa
pia amezitaka redio za jamii kuendesha mijadala kwa kuwashirikisha
wananchi na vyama visivyo vya kiserikali, kuhoji miradi ya maendeleo ya
taifa na kuchangia taarifa endelevu kwa maendeleo.
Akielezea
madhumuni ya warsha ya wadau wa mradi wa uchaguzi 2015, Afisa Miradi ya
Mawasiliano, Habari na Tehama wa shirika la kimataifa la sayansi, elimu
na utamaduni (UNESCO) Al Amin Yusuph, alisema kukutana kwa wadau
wakubwa wa uchaguzi kunalenga kukumbushana majukumu yaliyoko katika
uchaguzi hususan kujisajili kwa wapiga kura kutokana na mchango mkubwa
wa redio jamii katika kufikisha ujumbe, kuwa na dhamana, kuwahamasisha
na kuwaelimisha jamii na pia kuboresha sera za mtandao wa redio jamii
nchini.
“
Matatizo ya vitambulisho vipya elimu ni muhimu, kuhamasisha mchakato wa
demokrasia wananchi ambao uweo wao sio mkubwa kuwafikia hususan
wanawake ambao wanakosa fursa za kupiga kura na hawana nyenzo za kupata
habari, vijana nao hawapendi kujisajili na kupiga kura na vile vile kuna
vijana waliofikia umri wa kupiga kura, wote hawa wanahitaji elimu”.
Warsha
hiyo ya siku nne imeandaliwa kwa ushirikiano wa wadau wakubwa wa mradi
huo wa DEP ambao ni UNESCO, Ofisi ya msajili wa vyama vya siasa (RPP),
NEC na ZEC.
Warsha
hiyo pia inawashirikisha washiriki 31 wa mtandao wa redio jamii
Tanzania (COMNETA) unaotekeleza mradi wa demokrasia na amani kuelekea
uchaguzi mkuu 2015 unaofadhiliwa na mfuko wa mashirika ya maendeleo 10
ambayo ni Canada, Uingereza (DFID), Denmark, Umoja wa Ulaya na Finland.
Nyingine ni Ireland, Norway, Sweden, Switzerland na mfuko wa Umoja wa
Mataifa.
Makamu
wa Msajili wa vyama vya siasa nchini, Bw. Ibrahim Sapi Mkwawa, akitoa
salamu kutoka ofisi ya msajili wa vyama vya siasa inayoratibu mradi wa
uchaguzi unaolenga kuboresha demokrasia amani nchini (DEP) katika
kipindi hiki kuelekea uchaguzi mkuu ujao, unaofadhiliwa na Shirika La
Kimataifa la Maendeleo (UNDP) ) katika warsha ya siku nne inayoendelea
mjiji Dodoma.
Mtaalamu wa masuala ya uchaguzi kutoka UNDP, William Hogan akiwasalimia washiriki wa warsha hiyo.
Baadhi
ya maafisa kutoka ofisi ya msajili wa vyama vya siasa nchini
wakifuatilia mada mbalimbali zilizokuwa zikitolewa kwenye warsha hiyo
inayoendelea mjini Dodoma.
Afisa Habari na Mahusiano Tume ya Uchaguzi Zanzibar, Bi. Salha Ali,
akielezea mahusiano ya tume yake na vyombo vya habari vya jamii visiwani
Zanzibar.
Mshauri
na Mkufunzi kutoka Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na
Utamaduni (UNESCO) Bi. Rose Haji Mwalimu akihoji swali kwa watoa mada
wakati wa warsha hiyo ya siku nne inayoendelea mjini Dodoma.
Makamu
Mwenyekiti wa COMNETA ambaye pia ni Meneja wa Kituo cha Habari na
Mawasiliano cha Telecentre Sengerema FM mkoani Mwanza Bw. Felician
Ncheye akitoa maoni yake wakati wa kujadili mada mbalimbali zilizokuwa
zikiwasilishwa kwenye warsha hiyo.
Nuru H. Chuo kutoka Tandabui Health Access Tanzania/Afya Radio Mwanza akishiriki kuchangia maoni kwenye vikundi kazi.
Washiriki wakijadiliana kwenye vikundi kazi.
Khadija
Aboud kutoka Zanzibar Youth Organization Network (ZAYONET) akiwasilisha
kazi ya kikundi wakati wa warsha hiyo ya siku nne inayoendelea mjini
Dodoma.