Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimepata hati yenye shaka kutoka kwa Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) baada ya kupokea ripoti ya ukaguzi wa hesabu zake zinazoishia Juni 2011/12 na 2012/13
Ukaguzi huo ulifanyika kwa mujibu wa sheria namba 5
ya mwaka 1992 ya vyama vya siasa, iliyofanyiwa marekebisho na sheria
namba 7 ya mwaka 2009, unampa CAG mamlaka ya kukagua hesabu za vyama vya
siasa.
Katika ripoti hiyo kwa hesabu zilizoishia Juni 30,
2012, CAG ametilia shaka maeneo mbalimbali. Mkaguzi anasema katika
ripoti hiyo kuwa Chadema kilionyesha kina mali zenye thamani zaidi ya
Sh650 milioni, ambazo ni magari, mashamba, nyumba na pikipiki. Hata
hivyo, CAG anasema hakuona kitabu cha usajili wa mali hizo.
Pia, ripoti hiyo inaeleza kuwa Chadema ina akaunti
zaidi ya 200, ikijumlisha akaunti za makao makuu, kanda, mikoa, wilaya
na majimbo. Shaka ya mkaguzi ni kwamba hakuona salio la kufungia kitabu
likihusisha akaunti zote zinazotumia jina la Chadema.
Chadema kilitoa utetezi wake kuwa akaunti kuu ya
chama ndiyo inatoa fedha kwa akaunti za mikoani, hivyo wanaona mgao huo
wa fedha ni sehemu ya matumizi yao.
Mkurugenzi wa Fedha na Utawala wa Chadema, Anthony
Komu alisema Chadema iliwasilisha salio la akaunti kuu kwa kutambua
kuwa akaunti za mikoani zinapokea fedha kutoka makao makuu, hivyo
waliona hiyo ni sehemu ya matumizi yao.
“Chama chetu kimepokea taarifa aliyoitoa CAG na
tunaichukua kama sehemu muhimu ya kuboresha ujenzi wa chama chetu kama
taasisi ya kudumu na inayokua. Tutazifanyia kazi changamoto zote
alizoziainisha,” alisema Komu.
Aliongeza kuwa chama chake kinamtaka CAG aweke
bayana ni vyama vingapi havijakaguliwa na lini vitakaguliwa. Alivitaka
vyama vingine vilivyokaguliwa vitoe taarifa zao ili Watanzania wajue.
“Tunakumbuka CAG alitoa kauli bungeni kuwa si
vyama vyote vimekaguliwa. Kama sehemu ya jamii na chama kinachopigania
utawala wa sheria, aweke wazi ni vyama gani havijakaguliwa na kwa sababu
gani,” alisisitiza mkurugenzi huyo.
Mkurugenzi wa masuala ya Bunge na Halmashauri,
John Mrema alisema mpaka kufikia jana (juzi) walibaini kuwa Chama cha
Mapinduzi (CCM) kilikuwa hakijakaguliwa hesabu zake.
Alisema waliamua kupigania CAG kukagua hesabu za
vyama vya siasa kwa sababu mwaka 2005 walibaini kuwa CCM ilitumia fedha
za EPA katika kampeni zake. Aliongeza kuwa hawakutaka utamaduni huo
ujirudie.
“Kwa mujibu wa taarifa kutoka Kamati ya Bunge ya
Hesabu za Umma mpaka kufikia jana, CCM kilikuwa bado hakijakaguliwa,”
alisema Mrema na kuongeza kuwa chama chake kimeonyesha mfano licha ya
mapungufu yaliyobainika.
Alipouliza juu ya kukaguliwa kwa chama chake, Katibu wa Itikadi
na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye alisema Chadema wanakuja na jambo ambalo
lilishatolewa ufafanuzi siku nyingi. Alisema chama chake kilieleza na
kutoa vithibitisho kuwa walikaguliwa.
Nnauye aliongeza kuwa CAG pia alilitolea maelezo jambo hilo mara nyingi kusisitiza kuwa alishakikagua Chama cha Mapinduzi.
“Sasa hawa Chadema wamegeuka kuwa wasemaji wa CAG?
Kwanini nanyi msiende kumuuliza CAG juu ya jambo hili. Ina maana
mmeshasahau tuliyowahi kusema au aliyowahi kueleza CAG juu ya ukaguz?”
alihoji Nnauye na kusisitiza aulizwe CAG.
Hata hivyo, imebainika kuwa utekelezaji wa sheria
ya ukaguzi wa vyama vya siasa umeanza kutiliwa mkazo miaka ya hivi
karibuni, huku Chadema kikimsukuma CAG kufanya ukaguzi kila mwaka.
Kwa hesabu za mwaka ulioishia Juni 30, 2013,
ripoti ya CAG imetilia shaka kutoonekana kwa kitabu cha makusanyo ya
fedha chenye namba 451 – 500 kilichorekodiwa katika vitabu vyao kuwa
kilikusanya zaidi ya Sh31 milioni.
Kadhalika, mkaguzi mkuu alihoji ununuzi wa magari
10 ya CMC (Ford Rangers) bila kushirikisha kamati ya zabuni ambayo ndiyo
ina dhamana na manunuzi yote ya kichama.
Hata hivyo, Komu alifafanua kuwa uamuzi ulifanywa na kamati kuu na kamati ya katiba kupewa taarifa.
Hata hivyo, Komu alifafanua kuwa uamuzi ulifanywa na kamati kuu na kamati ya katiba kupewa taarifa.
Ununuzi wa jenereta lenye thamani ya Sh27.5
milioni unaelezwa zabuni haikutolewa kwa ushindani, jambo ambalo
mkurugenzi wa fedha alisema walifanya utafiti na kubaini kuwa ni kampuni
moja tu ndiyo ilikuwa na jenereta waliyoihitaji.