Na Raymond Mihayo
UCHAGUZI wa ndani wa Chama cha Chadema
wilayani Kahama mkoani Shinyanga umeingia dosari baada ya baadhi ya
wagombea na wanachama kuchapana makonde kupinga kuenguliwa kwa baadhi ya
majina ya wagombea katika uchaguzi wa Baraza la Vijana wa chama hicho
(BAVICHA).
Ugomvi huo ulitokea baada ya wagombea
waliopitishwa katika nafasi ya uenyekiti kuanza kujinadi kwa wanachama,
ndipo mgombea mmoja aliyeenguliwa (jina tunalo) kwa maelezo hana sifa
alipojitokeza kuzuia uchaguzi.
Kitendo hicho kiliungwa mkono na wafuasi wake wakiwemo wa kikundi cha ulinzi wa chama cha Red Brigade, na kuanzisha fujo.
Hali hiyo ilikwenda mbali zaidi kwani
wafuasi hao walianza kuwashambulia baadhi ya viongozi na wasimamizi
ambapo Mwenyekiti wa Chadema wa Halmashauri ya Msalala, Emmanuel Bombeda
alipigwa ngumi na vijana wa Red Brigade wanaomuunga mkono mgombea
aliyeenguliwa.
Hata hivyo, hali ilirejea kuwa shwari
baada ya Msimamizi wa Uchaguzi wa chama hicho Kanda ya Ziwa Mashariki,
Madata Benard Sande kuingilia kati na kuwataka wanachama kuwa wavumilivu
ili kufanikisha uchaguzi huo ikielezwa walioenguliwa hawakuonewa, kwa
mujibu wa Katiba ya chama hicho.
Katika uchaguzi huo, Diwani wa Kata ya
Naysubi, Leonard Mayala aliyekuwa anawania nafasi ya Mwenyekiti wa
Wilaya, naye alienguliwa, kwa sababu za kimaadili.
Baada ya kuzimwa kwa vurugu na uchaguzi
kuendelea, Juma Protas alichaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Chadema wilayani
Kahama, huku nafasi ya Katibu ikienda kwa Mshibu Peter. Kwa upande wa
Bavicha, Samwel Peter alichaguliwa kuwa Mwenyekiti.