Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), William Lukuvi amejikuta katika wakati mgumu mbele ya Rais Jakaya Kikwete baada ya kuzomewa hadi kukatisha hotuba yake akipingwa na wananchi pamoja na madiwani wa CCM wa Halmashauri ya Manispaa ya Dodoma alipokuwa akitetea kuwapo kwa Mamlaka ya Ustawishaji Makao Makuu (CDA).
Lukuvi alikumbana na mkasa huo wakati akijibu hoja
za Mbunge wa Dodoma Mjini (CCM), David Malole ambaye alitaka CDA
ivunjwe akiituhumu kuwavunjia wananchi nyumba bila kuwatafutia mahali pa
kuishi.
Hoja ya Malole kutaka CDA ivunjwe iliibuka katika
mkutano wa hadhara uliofanyika katika Kata ya Kikuyu, Manispaa ya Dodoma
baada ya Rais Kikwete kuzindua ujenzi wa Barabara ya Dodoma - Iringa.
Awali, mbunge huyo akitoa salamu kwa Rais Kikwete, alisema CDA imekuwa ni kero kwa wakazi wa mji huu.
“Mheshimiwa Rais, ni bora CDA ikafutwa na ardhi
ikarudishwa kwa halmashauri kwa kuwa hakuna kitu kinachofanyika. Ipo
miji mingi ambayo haina CDA lakini imekuwa majiji. Leo hii zaidi ya
miaka 40 CDA imeshindwa kuufanya Mji wa Dodoma kuwa jiji,” alisema na
kuongeza:
“Licha ya kuwa CDA jukumu lake ni kuhakikisha
inapima viwanja na kupanga ustawi wa mji lakini imeshindwa kufanya
hivyo, jambo ambalo linawakera wananchi wa Dodoma na kusababisha
kukichukia Chama Cha Mapinduzi na Serikali yao,” alisema.
Kutokana na hoja hiyo kushangiliwa na madiwani
pamoja na wana CCM na wananchi wengine, Malole aliendelea kufafanua kuwa
suala la kupigania wananchi wapate viwanja linamuweka katika hali ngumu
kwa sababu anatishiwa kuwa hatapata nafasi ya kugombea ubunge tena.
“Mimi nasema, ikimpendeza Mungu kuwa mbunge
nitaendelea kuwa mbunge na kama siyo mpango wa Mungu basi, kwani kuna
propaganda nyingi juu yangu lakini hiyo yote ni kutokana na kupigania
wananchi wapewe haki zao,” alisema.
Kuzomewa
Baada Malole kutoa madai hayo, Lukuvi ambaye ni
Mwenyekiti wa Bodi ya CDA alilazimika kupanda jukwaani ili asawazishe
kauli za mbunge huyo, jambo ambalo liliibua zogo na wananchi kuzomea.
Zomeazomea dhidi ya Lukuvi ilitawala katika
kipindi chote alichokuwa jukwaani huku viongozi wa chama wakihaha
kuwazuia wanachama na madiwani wa CCM wasizomee bila mafanikio.
Hali iliendelea kuwa mbaya kwa Lukuvi pale aliposema, “Mimi ni
mdau mkubwa wa CDA na ni kati ya watu ambao walishiriki kupeleka
maendeleo katika Mji wa Dodoma.”
Kauli hiyo ilisababisha madiwani pamoja na
wananchi kuanza upya kumzomea huku wakimtaka ashuke jukwaani kwa madai
kuwa hana cha kuwaeleza hadi wamwelewe.
Hali hiyo iliambatana na nyimbo zilizoanzishwa na
madiwani, “CCM.. shuka chini, CCM shuka chini” hali iliyomfanya Lukuvi
kushuka jukwaani.
Baadaye Rais Kikwete akizungumza na wakazi hao,
alitoa siku saba kwa viongozi wa mkoa kwa kushirikiana na mbunge kukaa
na kutatua mgogoro huo na aliahidi kukutana nao Septemba 8, mwaka huu.
Alisema migogoro haiwezi kutatuliwa katika
mikutano ya hadhara, bali vikao vya kazi. Aliwataka kukutana kuangalia
ni jinsi gani watamaliza mgogoro huo bila kuwa na fujo wala lawama.
