Watu wawili wamekufa na wengine watano kujeruhiwa baada ya magari mawili, likiwamo basi dogo la abiria walilokuwa wakisafiria kugongana uso kwa uso na lori la mafuta.
Kwa
mujibu wa Kaimu Kamanda wa Polisi mkoani Pwani, Athuman Mwambalaswa
alisema kuwa tukio hilo lilihusisha gari aina ya Toyota Coaster
lililokuwa linatokea kwenye msiba Musoma mkoani Mara kwenda Dar es
Salaam na kugongana na lori la mafuta.
Kamanda
Mwambalaswa alisema kuwa ajali hiyo ilitokea juzi maeneo ya Ubena Senge
katika barabara ya Morogoro, chanzo kikitajwa kuwa ni uzembe wa gari
dogo aliyehama upande wake kutokana na kile kilichoelezwa kuwa ni uchovu
wa safari ndefu.
Alisema
basi dogo lenye namba za usajili namba T 663 BKP lililokuwa
likiendeshwa na Ally Abdul (34), likiwa na abiria 20 liligongana na lori
la mafuta aina ya Leyland Daf lenye namba za usajili T 858 CLK na tela
namba T 421 CKY, mali ya kampuni ya Ramader ya Dar es Salaam ambalo
dereva wake ametajwa kwa jina moja la Rashid.
Aliwataja
waliokufa kwenye ajali hiyo kuwa ni Neema Mile (39) na Jane Mtani (38)
ambao miili yao imehifadhiwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Pwani,
Tumbi ambako pia majeruhi wamelazwa.
