Mwanariadha mlemavu wa Afrika Kusini Oscar Pistorius, amepatikana na hatia ya kumuua mpenziwe Reeva Steenkamp bila kukusudia.
Akitoa uamuzi wake jaji Thokozile Masipaal alisema kuwa mwanariadha
huyo alimuua Reeva kwa bahati mbaya alipofyatua risasi kupitia kwa
mlango wake wa choo akiwa katika hali ya mshtuko akidhani kuwa jambazi
aliyekuwa amevamia nyumba yake.
Alisema kuwa upande wa mashtaka umeshindwa kuthibitisha kuwa
Pistorius alinuia kumuua Steenkamp na hakutekeleza mauaji hayo kwa
makusudi.
Pia alipatikana na hatia ya kosa la kutumia silaha yake visivyo alipokwenda mgahawani jijini Johannesburg.
Kwa uamuzi huo wa jaji, Oscar atahukumiwa miaka michache zaidi ya jela
tofauti na kama angepatikana na hatia ya kuua kwa kukusudia.
Hukumu ya kuua bila kukusudia nchini Afrika Kusini ni hadi miaka 15
jela. Jaji Masipa aliamua kuwa waendesha mashtaka wa serikali
walishindwa kutoa ushahidi wa kutosha kuwa alimuua mpenzi wake kwa
kukusudia.
