MKUTANO wa Rais Jakaya Kikwete na viongozi wa juu wa vyama vya siasa uliofanyika jana mjini Dodoma umetajwa kuwa na dalili nzuri zinazoashiria mwafaka utapatikana juu ya mchakato wa utengenezaji Katiba mpya.
Kikwete
alikutana jana na vyama hivyo kupitia Kituo cha Demokrasia Tanzania
(TCD) kinachoongozwa na Mwenyekiti wa UDP, John Cheyo kukiwa na ajenda
mbili mojawapo ikihusu mchakato unaoendelea wa kutengeneza Katiba mpya.
TCD
inaundwa na vyama vyenye uwakilishi bungeni, ambavyo ni CCM, CUF,
CHADEMA, TLP, NCCR-Mageuzi na UDP. Ingawa yaliyojiri ndani ya mkutano
huo unaotajwa ulijaa amani na ucheshi hayakuwekwa wazi, Cheyo ambaye ni
Mwenyekiti wa TCD alisema ajenda nyingine ilihusu Uchaguzi Mkuu wa mwaka
2015.
Akizungumza
na mwandishi wa habari hizi, Cheyo alisema mkutano huo ulienda vizuri
na wamekubaliana Septemba 8, mwaka huu, kukutana kwa mazungumzo zaidi
ambayo anaamini kutakuwa na matokeo chanya.
“Mkutano
umeenda vizuri sana…ulikuwa mkutano mzuri sana, ulijaa amani na
ucheshi. Tumekubaliana kwamba tunakutana tarehe 8, Septemba,” alisema Cheyo.
Akielezea
imani yake juu ya mkutano huo wa wiki ijayo katika suala zima la kupata
mwafaka juu ya mchakato wa Katiba mpya, baada ya Kundi la Umoja wa
Katiba ya Wananchi (Ukawa) kususa, Cheyo alisema, “…kukubaliana kukutana tu, ni jambo muhimu sana na lenye dalili nzuri.”
Kwa
mujibu wa Cheyo, mkutano huo ulitawaliwa na utulivu, ucheshi jambo
ambalo anaamini utamaduni wa Watanzania wa kukaa na kuzungumza utazaa
matunda katika mkutano ujao.
Cheyo
ambaye alishiriki pamoja na Katibu wa chama chake, Isack Cheyo, alisema
wanachama wote wa TCD akiwemo mwakilishi wa vyama visivyo na wabunge,
walihudhuria na kushiriki mkutano huo kwa ufasaha.
Kwa
upande wa CCM, walioshiriki ni Makamu Mwenyekiti Bara, Philip Mangula
na Katibu Mkuu, Abdulrahman Kinana. Chadema aliyeshiriki ni Katibu Mkuu
wake, Dk Wilbrod Slaa pamoja na Mwanasheria wa chama hicho, Tundu Lissu.
Washiriki wengine ni Mwenyekiti wa Chama cha NCCR Mageuzi, James Mbatia na Katibu Mkuu wake, Mosena Nyambabe.
CUF iliwakilishwa na Mwenyekiti wake, Profesa Ibrahim Lipumba na Naibu Katibu Mkuu Bara, Magdalena Sakaya.
Kwa upande wa TLP, Mwenyekiti wake, Augustino Mrema na Katibu Mkuu wake, Jeremiah Shelukindo walishiriki.
Aidha
Mwenyekiti wa United Peoples Democratic Party (UPDP), Fahmi Dovutwa
aliwakilisha vyama visivyo na wabunge katika TCD. Cheyo alisema kabla ya
mkutano huo wa wiki ijayo, Septemba 6 na 7, TCD itakuwa na mkutano wake
mkuu utakaokutanisha wanachama kabla ya kesho yake kukutana na Rais.
Ajenda
kuhusu mchakato wa Katiba mpya, unazingatia hali ya sasa ya kisiasa
ambayo, kundi la Ukawa lilisusa Bunge Maalumu la Katiba kwa madai ya
kutoridhishwa na mwenendo wake.
Tangu
Ukawa wasuse Bunge hilo linaloendelea mjini Dodoma, wananchi na makundi
mbalimbali ya kijamii yamekuwa yakitaka wajumbe hao waliosusa warejee
bungeni kuungana na wenzao waliobaki kutengeneza Katiba yenye
maridhiano.
Licha
ya kuwepo sauti za kusihi kundi hilo kurejea bungeni, pia wapo ambao
wamekuwa wakisisitiza maridhiano kati ya Ukawa na Tanzania Kwanza
yapatikane ili kuunda Katiba yenye ushiriki wa makundi yote.
Wadau
wengine, likiwemo Jukwaa la Wakristo Tanzania lililotoa taarifa yake
jana kuhusu mchakato wa Katiba, na kumwomba Rais Kikwete asitishe Bunge
hilo ili upatikane mwafaka na maridhiano.
Katika
taarifa ya jukwaa hilo linalojumuisha Baraza la Maaskofu Tanzania (TEC)
Baraza la Makanisa ya Pentekoste (CPCT), Jumuiya ya Kikristo Tanzania
(CCT) na Kanisa la Waadventista Wasabato, limeomba mchakato uahirishwe
kuepusha athari kwa mshikamano na umoja wa taifa.
Mjadala
bungeni kesho BUNGE Maalumu la Katiba litaanza majadiliano kesho baada
kamati zote kumaliza kupitia na kuchambua sura zote za Rasimu ya Katiba.
Jana na leo kwa mujibu wa Katibu wa Bunge hilo, Yahya Hamad kamati hizo
ilikuwa ziwasilishe taarifa zao kwa Sekretarieti ya Bunge ambayo
itaanza kuzichambua kabla ya kuzipeleka kwenye Bunge.
Hamad
alisema licha ya kuzichambua, Kamati ya Uongozi itakutana leo kwa ajili
ya kujadiliana mambo mbalimbali kabla ya majadiliano kuanza kesho.
"Ratiba
yetu inaonesha kuwa Jumanne (kesho) Bunge lote litakutana kwa ajili ya
majadiliano ambayo ni muhimu sana ili kuwekana sawa," alisema Hamad.
Alisema siku 15 zimepangwa kwa ajili ya majadiliano ili taarifa hizo
pamoja na maoni ya wajumbe wakati wa mjadala yawasilishwe kwa Kamati ya
Uandishi wa Rasimu ya Katiba.
Hamad
alisema Bunge hilo likishakamilisha mjadala, ndipo Kamati ya Uandishi
wa Katiba ambayo iko chini ya Mwanasheria maarufu Andrew Chenge itaanza
kazi ya kuandika Rasimu ya Katiba.
Alisema
Kamati ya Chenge pia italazimika kurejesha Rasimu hiyo ndani ya Bunge
kuona kile walichokiandika ni sahihi kabla ya kupigiwa kura na wajumbe
wote. Bunge hilo limehitimisha siku 30 ambazo walizitumia kwa kamati
mbalimbali kujadili Rasimu ya Pili ya Katiba iliyowasilishwa bungeni
hapo na Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba.
Kwenye
majadiliano hayo, kamati mbalimbali zilitupilia mbali baadhi ya
mapendekezo yaliyoko kwenye Rasimu ya Katiba ikiwemo lile linalotaka
wabunge wawe na ukomo na wananchi kupewa haki ya kumwondoa mbunge wao
madarakani.
Eneo
lingine ambalo baadhi ya kamati ziliyakataa ni ambayo yalitaka baadhi
ya wateule wa Rais kutakiwa kuthibitishwa na Bunge kwa maelezo kuwa
viongozi wanaotakiwa kuthibitishwa na chombo hicho, ni wale tu
wanaowajibika kwa Bunge hilo.
Lakini
pia kuna mvutano wa aina ya Bunge litakaloundwa kutokana na baadhi ya
wajumbe kutaka mambo ya Tanzania Bara yajadiliwe na Watanzania Bara tu
na pia yawepo mambo ya Muungano ambayo yatajadiliwa na wabunge kutoka
pande zote za Muungano.
Hoja
ya uraia pacha pamoja na suala la Kadhi Mkuu nalo ni miongoni mwa
yanayodaiwa kukabiliwa na mvutano ndani ya baadhi ya kamati.
