Aliyekuwa kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, marehemu ACP Liberates Barlow (53) enzi za uhai wake.
Ikiwa imepita takribani miaka miwili tangu aliyekuwa Kamanda wa Polisi
Mkoa wa Mwanza, ACP Liberates Barlow (53) (picha ndogo) afariki dunia
usiku wa Oktoba 13, 2012 kwa kupigwa risasi na watu waliodhaniwa ni
majambazi, mke wa marehemu, Stella Barlow naye yamemkuta mazito kwani
chupuchupu auawe.
Kwa mujibu wa chanzo chetu, Jumatano ya Agosti 13, mwaka huu mjane
huyo anayeishi jijini Mwanza alikwenda Moshi Vijijini mkoani Kilimanjaro
kwenye kaburi alilozikwa mumewe kwa ajili ya kulijenga lakini cha ajabu
ndugu wa marehemu walimfukuza kwa mapanga na marungu na kumtaka aondoke
eneo hilo mara moja.
Chanzo kilisema kuwa, ndugu hao walimfukuza
huku wakidai kwamba awalipe pesa kwa ajili ya eneo hilo la kaburi
alilozikwa mumewe kwa vile marehemu hakuzikwa kwenye eneo lake, jambo
ambalo ilidaiwa kuitia aibu familia hiyo.
Uwazi lilimsaka msemaji wa ukoo bila mafanikio lakini mtu mmoja
aliyedai si msemaji akiomba kuhifadhiwa jina lake alisema kilichotokea
ni mwanamke huyo kutaka kuonesha anajua sheria wakati ukoo ulitaka kila
kitu kiende kwa uzuri na utaratibu.
“Sisi hatukuwa na nia mbaya, kila mtu
anajua mila za Kilimanjaro, sasa tulitaka kuweka mambo sawa, yeye akawa
anataka kutuonesha anajua sheria,” alisema mtu huyo.
Juzi, Uwazi lilimsaka kwa njia ya simu mjane wa marehemu huyo ambapo alipopatikana alikuwa na haya ya kusema:
“Ni kweli tukio hilo lilitokea nilikwednda kwenye kaburi la mume
wangu kwa ajili ya kufanya maombi lakini nilizuiliwa na ndugu wakisema
kwamba hawataki kuniona kwa sababu mume wangu alizikwa pale kimakosa.
“Hata hivyo, walinitimua huku wengine wakinitishia kwa mapanga lakini sijachukua hatua yoyote ila nimemwachia Mungu.”
CHANZO:UWAZI/GPL