CHADEMA YACHARUKA, YATAKA KUNI NA MKAA VIRUHUSIWE KUTUMIKA BILA VIKWAZO

CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) katika Wilaya ya Kibondo mkoani Kigoma, kimeitaka Halmashauri ya Wilaya hiyo kupitia Idara ya Misitu kuondoa zuio la uuzaji wa mkaa na kuni kwa wachuuzi wadogo wadogo ili kuepuka usumbufu kwa jamii. 

Mwenyekiti wa chama hicho wilayani humo, Nikolaus Kilunga, amesema wakazi wengi wa Kibondo mjini na vijijini wanatumia nishati ya mkaa na kuni hivyo kauli ya serikali kuwazuia ghafla bila kufanya maandalizi ni kuwapa adha wananchi wanaotegemea nishati hiyo. 

“Tunapenda kutoa tamko la kupinga uamuzi wa Halmashauri kuzuia uuzaji wa mkaa na kuni bila kuwa na maandalizi ya kutosha kwa kutoa taarifa kwa wahusika, kwani hawajatoa elimu wala kuangalia athari za kiuchumi na kijamii kwa wakazi wa wilaya nzima ya Kibondo zinazoweza kutokea mara baada ya kufanya maamuzi kama haya” alikaririwa

Aidha, ameeleza kuwa kwamba wameieleza idara husika kuhakikisha inakaa pamoja na wauzaji na watumiaji wa mazao hayo, sambamba na kutoa elimu juu ya namna ya utunzaji wa mazingira pamoja na tozo wanazotakiwa kutoa ili wananchi waweze kuelewa jambo wanalolifanya. 

Katika hatua nyingine, chama hicho kimetoa siku saba (7) kwa serikali kubatilisha maamuzi yake na kukaa na wadau wote ikiwa ni pamoja na watumiaji na wauzaji wa mkaa na kuni, ili kutoa elimu ya mali zinazozunguka wananchi na namna ya kuzitumia, elimu ya kodi na tozo nyingine ili kuepusha mzozo usio wa lazima kwa wananchi wanaopata kipato kidogo kutokana na kutegemea mazao hayo.

 Wananchi wa Wilaya hiyo wakiongea kwa nyakati tofauti leo Agosti 25, 2014, wamedai serikali kuendeleza zuio hilo bila utaratibu maalumu ni ukiukwaji wa haki za binadamu na kuwanyima wananchi mahitaji ya lazima kwani hawataweza kupika kutokana na kutegemea kuni na mkaa kwa ajili ya kupikia na kuuza kwa ajili ya kujitafutia kipato cha familia zao. 

Kwa upande wa wafanyabiashara wa mkaa mkoani humo akiwemo Jovita Nyuntwa, wamesema hatua hiyo imewafanya waishi kwa kuhangaika kutokana na kupewa muda mfupi wa kuacha kufanya biashara hiyo Agosti 22, 2014 huku wakisema watumiaji wa nishati hiyo wameonekana kupata adha kubwa kutokana na kusitishwa kwa huduma hiyo. 

Meneja Misitu katika Wilaya hiyo, Rojas Simon, amekiri kuwepo kwa suala hilo na kusema “Mimi suala langu ni kuhakikisha ninasimamia kuwa sheria inafuatwa na ninapenda nirudie kwamba hatujamzuia mtu kufanya biashara ya mkaa bali tunamruhusu mtu ambaye amefuata taratibu za sheria za misitu ili afanye biashara na siwezi kumuacha mtu akavunja sheria kwasababu eti kuna hali ngumu ya maisha". 

Nishati ya mkaa na kuni katika Wilaya ya Kibondo mkoani humo, imeonekana kuuzwa kwa magendo na kwa bei ya juu kati ya shilingi 44,000 kwa gunia hadi shilingi 50,000 hali ambayo imelalamikiwa na baadhi ya wauzaji na watumiaji kabla ya zuio hilo.

CHANZO:FikraPevu


JIUNGE NA EDMO BLOG SASA

Usipitwe!! Jiunge nasi kupitia Facebook,Twitter na Instagram ili kupata habari zote za town! Usikose kujiunga na Youtube kuangalia video zote kali kutoka Edmo Blog Pekee!, kujiunga bonyeza hapa>>>Youtube

Tupe Maoni Yako lakini Usiandike Matusi



 
© Copyright EDMO BLOG | Designed By Peruzibongo