Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM bara), Mwigulu Nchemba ameutaka Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), kurejea bungeni ili kukamilisha Mchakato wa Katiba Mpya kwa amani na utulivu.
Rai hiyo imekuja wakati mijadala mbalimbali
inaendelea juu ya hatima ya wajumbe hao na mchakato huo tangu walipotoka
bungeni na kususia vikao vya Bunge hilo Aprili 17 na kukataa kurejea,
huku zikiwa zimesalia siku tisa kabla ya Bunge hilo kuendelea na vikao
vyake mjini Dodoma Agosti 5.
Akihutubia mkutano wa hadhara wa chama hicho mjini
Mwanza jana, Nchemba alisema:“Natoa rai kwa wenzetu…turudi ili tupate
majibu ambayo ni Katiba Mpya. Tuachane na haya mambo.”
Naibu huyo alisema: “Huu ndiyo wakati wa
kutengeneza Katiba ambayo itakuwa Sheria mama itakayotumika kwa miaka 50
ijayo, hivyo wajumbe hao lazima wazingatie jambo hilo.”
“Halafu wanasema tuache..kwa nini tuache wakati hatujafikia sehemu ya kujadili mambo yanayowahusu Watanzania,” aliohoji Nchemba.
Alisema kuwa, badala ya kuendelea na mgomo huo ni
vyema wajumbe hao wangeweka wazi nia yao tangu machakato huo ulipoanza
kuliko mambo wanayoyafanya sasa huku gharama nyingi zikiwa zimeshaumika
kwa ajili ya kuendesha mchakato wa Katiba Mpya.
“Tumeshatumia fedha nyingi, zaidi ya Sh7 bilioni
pamoja na zile zilizotegwa ili kukamilisha mchatako huu wa siku 130 za
shughuli hizo. Ikumbukwe kuwa fedha hizo ni kodi za Watanzania ambao
wamekuwa wakisubiri kwa hamu mchako umalizike ili wapate Katiba
wanayoitaka,” alisema.