| Kamanda wa polisi mkoa wa Shinyanga SAC Justus Kamugisha akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake leo mchana |
Siku
moja tu baada ya abiria 63 kunusurika kufa baada ya basi la
Supernajimunisa lilikitoka Mwanza kwenda Dar es salaam kupinduka huko
Usanda Shinyanga,leo
wafanyabiashara
watatu wamefariki dunia na wengine 46 kujeruhiwa baada ya lori aina ya
Fuso walilokuwa wanasafiri na bidhaa zao kuacha njia na kupinduka katika
kijiji cha Uchunga wilayani Kishapu.
Ajali
hiyo imetokea leo saa tatu asubuhi baada ya lori lenye namba za usajili
T680 ARL aina ya Fuso lililokuwa limepakiza mizigo na wafanyabiashara
ambao idadi yao bado haijajulikana likitokea kijiji cha Kiloleli
wilayani Kishapu kwenda katika mnada wa Mhunze uliopo Kishapu.
Kamanda
wa polisi mkoa wa Shinyanga Justus Kamugisha amesema katika taarifa za
awali ajali hiyo imetokana na mwendo kasi wa gari gari
hilo aina ya fuso mali ya Ngasa Seni mkazi wa Kiloleli lililokuwa
likiendeshwa na Shija Ngasa mfanyabiashara ,mkazi wa Kiloleli wilayani
Kishapu ambalo lilimshinda dereva na kuacha njia kisha kupinduka na kusababisha vifo na majeruhi.
“Hili gari ni lori linatumika kubeba mizigo lakini,lilikuwa limepakiza abiria ,wengi ni wafanyabiashara,lilikuwa linatoka Kiloleli kwenda Mhunze mnadani,liliacha njia na kupinduka,dereva alitoroka baada ya kutokea ajali hiyo na anatafutwa na jeshi la polisi.
Watu
waliopoteza maisha mpaka sasa ni watatu,majeruhi 46, 35 na wanapata
matibabu katika hospitali ya mkoa wa Shinyanga na 11 katika hospitali ya
Kolandoto,japokuwa kuna taarifa kuwa majeruhi wanaweza kuongezeka kwani
wengine walipelekwa Kishapu.
Kamanda
Kamugisha ametoa wito kwa wamiliki wa magari,wananchi wakiwemo
wafanyabiashara kuacha tabia ya kutumia magari yasiyo ya abiria
kusafiria.
Amewashauri
wafanyabiashara kubadilika na kuacha ubahiri wa kupenda vitu rahisi
hivyo wawe wanapanda magari ya abiria badala ya kupanda magari ya
mizigo.
Kaimu
mganga mfawidhi wa hospitali ya mkoa wa Shinyanga Dkt Maguja Daniel
amesema wamepokea miili miwili ya marehemu na mwingine mmoja alifariki
wakati akipatiwa matibabu na majeruhi 35 na wanaendelea kupatiwa
matibabu katika hospitali hiyo.
Na Kadama Malunde-Malunde1 blog
