Jeneza lenye mwili wa marehemu Daniel Lema kabla ya kuagwa.
Daniel Anael Lema, aliyekuwa mwanafunzi wa mwaka wa nne wa shahada ya
sheria katika Chuo Kikuu Kishiriki cha Mt. Augustino, Tawi la Iringa
(Ruaha University College - RUCO), amefariki dunia baada ya kushambuliwa
kisha kuchomwa moto na wananchi wenye hasira akidhaniwa kuwa mwizi.
Tukio hilo lilitokea Juni 24, 2014, majira ya saa 5 usiku ambapo
inadaiwa kuwa Daniel alikuwa ametoka kuangalia michuano ya Kombe la
Dunia, akawa anatafuta chakula cha jioni ambapo alipofika kwenye mgahawa
mmoja ambao ulikuwa umefungwa, aliingia ndani ambapo binti aliyekuwa
amelala ndani ya mgahawa huo, alianza kupiga kelele za mwizi
zilizowakusanya wananchi wenye hasira kali.
Wananchi hao
walianza kumshambulia Daniel wakiongozwa na mlinzi mmoja wa jamii ya
Kimasai, baada ya kuzidiwa na kichapo wananchi hao walimmwagia mafuta ya
taa na kumchoma moto kisha wote wakatoweka.
Mwanafunzi huyo aliokolewa na madereva bodaboda ambao walizima moto
na kumkimbiza katika Hospitali ya Rufaa ya Iringa lakini siku kadhaa
baadaye alifariki dunia.
Mwili wa marehemu umeagwa mapema leo
katika hospitali hiyo tayari kwa safari ya kuelekea mkoani Kilimanjaro
kwa ajili ya mazishi yatakayofanyika kesho Jumatano.
Daniel Anael Lema, aliyekuwa
mwanafunzi wa mwaka wa nne wa shahada ya sheria katika Chuo Kikuu
Kishiriki cha Mt. Augustino, Tawi la Iringa (Ruaha University College -
RUCO) enzi za uhai wake.Ndugu wa marehemu wakiandaa jeneza kwa ajili ya mwili wa marehemu Daniel kuagwa.