Serikali imepiga marufuku tabia ya askari Polisi wa Kikosi cha Usalama Barabarani, kuvizia magari katika barabara kuu wakiwa na kifaa cha kupima mwendo kasi wa magari.
Naibu
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Peraira Silima, alisema tabia hiyo ya
trafiki ni kinyume cha sheria na zinaweza kusababisha ajali.
Hata
hivyo, Silima aliwataka madereva kutii Sheria za Barabarani ikiwemo
kupunguza mwendokasi na kufafanua kuwa, wakati mwingine askari hutafuta
kivuli na hatua hiyo isichukuliwe kuwa wanavizia magari.
Katika
swali lake, Ngoye alitaka Serikali ieleze ni hatua gani zimekuwa
zikichukuliwa kuhakikisha madereva wanafuata sheria zilizowekwa kama
inavyofanyika katika nchi nyingine.
Ngoye
pia alitaka Serikali ieleze kwa nini madereva wameendelea kutumia
magogo, mawe na majani yenye miba barabarani kuashiria kuwa kuna gari
limeharibika, na wakiondoka wanayaacha na wengine wameendelea kuendesha
magari huku wakisikiliza simu.
Naye
Mbunge wa Musoma Mjini, Vincent Nyerere (Chadema), alihoji kama ni
sahihi kwa trafiki kuvizia magari na kifaa cha kupima mwendo kasi.
Akifafanua
majibu ya maswali hayo, Silima alisema trafiki kujificha na chombo
hicho na kujitokeza kusimamisha gari ni kinyume cha sheria kwa kuwa
tabia hiyo inaweza kusababisha ajali.
Kuhusu
matumizi ya magogo, majani na mawe, alisema ni kinyume na Sheria na
kutaka madereva watumie alama za pembe tatu ambazo ni nzito na kuachana
na alama hizo ambazo ni nyepesi ambazo hupeperushwa na upepo.
Silima
pia alionya kuwa Serikali iko mbioni kuanza kuwanyang’anya leseni za
udereva madereva wote ambao watathibitika kukithiri kwa makosa ya
usalama barabarani, na kuzuiwa kabisa kufanya kazi hiyo.
Hatua
hiyo itaanza kuchukuliwa mara baada ya kukamilika na kuanza kwa Mfumo
mpya wa Nukta, ambao utaweka kumbukumbu za makosa ya madereva ambayo
itatumika kuwachukulia hatua hiyo.