Denti mmoja wa kike wa darasa la saba anayesoma katika Shule ya
Msingi Chanzige B iliyopo Kisarawe, Pwani amejikuta katika wakati mgumu
baada ya kulawitiwa na kusababishiwa maumivu makali sehemu zake za siri.
Simulizi ya binti huyo inayouma sana, inaeleza kuwa denti huyo
alifanyiwa unyama huo na vijana watatu ambao bado hawajafahamika majina
yao mara moja lakini amekuwa akimtaja mmoja kwa jina la Musa.
Tukio
hilo lenye sura ya majonzi hasa kwa wazazi na watoto, lilitokea hivi
karibuni Kisarawe mkoani Pwani lakini ilifanywa siri kwa muda mrefu na
mtoto huyo kukaa bila matibabu.
Chanzo chetu cha habari kinasema kuwa, shangazi wa mtoto huyo ambaye
anaishi naye ndiye sababu ya kutopata tiba, kwani anadaiwa kuchukua
kiasi cha shilingi 200,000 kutoka kwa Musa anayetajwa kuwa mmoja wa wahusika
kama kifunga mdomo.
“Haya mambo yametokea muda tu na huyo mtoto (anamtaja jina lakini
linahifadhiwa) alimwambia shangazi yake kuwa huyo Musa na wenzake
wanahusika, lakini cha ajabu walikutana huko na kupeana hizo fedha ili
mambo yaishe.
“Hii haikubaliki kabisa. Unajua huyo shangazi mtu
anafanya hivyo kwa sababu si mwanaye, ingekuwa ni damu yake kweli
asingeweza kufanya kitu cha namna hiyo,” kilipasha chanzo hicho na
kuongeza:
“Ilibaki
kidogo mtoto ashindwe kufanya mtihani wake wa Mock kwa sababu ya tukio
hilo. Kiukweli si jambo la kulifumbia macho. Huyo mama (shangazi)
anatakiwa kuchukuliwa hatua za kisheria.”
Chanzo hicho kikazidi
kusema kuwa, awali kesi hiyo ilifikishwa katika Kituo cha Polisi
Kisarawe na kufunguliwa jalada lakini shangazi wa mtoto huyo aliamua
kuyamaliza mambo hayo na mmoja wa watuhumiwa baada ya kupewa kiasi hicho
cha fedha.
Uchunguzi wetu umegundua kuwa, sakata hilo liliripotiwa katika
Kituo cha Polisi Kisarawe na kufunguliwa jalada nambari KIS/RB/326/2014,
ambapo Fomu ya Polisi Nambari 3 (PF3) ilitolewa kwa ajili ya matibabu
ya mtoto huyo.
Akisimulia zaidi, mama mzazi wa mwanafunzi aitwaye
Mariam Said alisema, alipata taarifa za mwanaye kukumbwa na masahibu
hayo ambapo aliamua kusafiri kutoka Mlandizi anapoishi hadi Kisarawe
kufuatilia tukio hilo.
“Inaniuma sana mwanangu kufanyiwa unyama halafu mambo yanamalizwa
kienyeji. Nilikuja hadi hapa, nikamwuliza shangazi yake na binti yangu
juu ya tukio hilo, akakiri lakini akasema eti mwanangu hakuwa mkweli
mapema.
“Nikaamua kwenda polisi mimi na ndugu zangu wengine. Tulipouliza hiyo kesi kituoni hapo, tukaambiwa ni kweli ilifungiliwa na
nikatajiwa RB (ile iliyoandikwa hapo juu). Polisi wakatuambia,
walishangaa kuona mlalamikaji harudi tena na hata PF3 waliyotoa
haikurudishwa tena baada ya kuondoka,” alisema Mariam.
Binti
huyo alisema alifanyiwa ukatili huo wakati akitokea shuleni na kwamba
alimweleza shangazi yake kila kitu kuhusiana na tukio hilo kabla ya
kwenda naye polisi kutoa taarifa.
“Baada ya hapo tulikwenda katika Hospitali ya Kisarawe lakini
sikupata matibabu kwa sababu shangazi alisema hana pesa ya malipo, tukarudi nyumbani na kununua dawa kwenye maduka ya dawa,’’ alisema mtoto
huyo na kuongeza:
“Pale hospitalini, shangazi alitakiwa kutoa kadi
ya Bima au shilingi 10,000 ili nitibiwe. Sasa hakuwa na Bima wala hiyo
pesa ndiyo maana ikashindikana.”
Amani lilifunga safari hadi Shule ya Msingi Chanzige B na
kuzungumza na Mwalimu Mkuu, Issac Eliah ambaye alikiri kupokea taarifa
ya mwanafunzi wake kubakwa na kulawitiwa kutoka kwa shangazi wa mtoto
huyo na kutoa ruhusa kwa ajili ya matibabu.
Shangazi wa mtoto huyo alipotakiwa kuzungumzia ishu ya kuzima kesi
hiyo kwa madai ya kupewa shilingi 200,000 alisema: “Mimi sitaki
kuzungumzia suala hilo, nendeni polisi mkaulize siyo kuniuliza mimi.”
Credit: Amani/ Gpl