Wiki
mbili baada ya kuitwaa rasmi Ikulu ya Malawi, Rais mpya wa nchi hiyo,
Profesa Peter Mutharika anatarajiwa kufunga ndoa na Gertrude Maseko
Jumamosi ijayo, baada ya kuishi maisha ya ukapera kwa zaidi ya miaka 30.
Mutharika,
mdogo wa Rais wa Pili wa Malawi, Bingu wa Mutharika ambaye kwa sasa ni
marehemu, alikuwa mume wa Christophine G. Mutharika, raia wa Visiwa vya
Carribean na kubahatika kuzaa naye watoto watatu, Monique, Moyenda na
Mahopela ambao wote ni wanasheria mahiri kwa sasa nchini Marekani.
Hata
hivyo, Mutharika alimpoteza mkewe huyo kwa ugonjwa wa kansa mwaka 1990,
hivyo kumfanya asioe kwa muda mrefu, huku akijikita zaidi katika kazi
zake za uwakili kwa zaidi ya miaka 40 nchini Marekani.
Kwa
mujibu wa taarifa ya Ikulu ya Malawi iliyosainiwa na Mwandishi wa
Habari wa Rais, Chikondi Juma imeeleza kuwa ndoa ya Rais Mutharika na
Maseko itafungwa Jumamosi ya Juni 21 mwaka huu katika Kanisa la
Mtakatifu Michael na Malaika Wote, jijini Blantyre.
Harusi
hiyo inafanyika huku Wamalawi wakifanya chereko za kuwasili kwa mara ya
kwanza nchini Malawi kwa mabinti wa rais huyo, Monique na Moyenda, siku
chache baada ya uchaguzi uliomwingiza Ikulu baba yao akiwa Rais wa Tano
wa nchi hiyo.
Taarifa
hiyo ya Ikulu imeongeza kuwa, Maseko ambaye alikuwa mbunge wa jimbo la
Balaka Kaskazini kwa tiketi ya chama cha Democratic Progress (DPP) cha
Mutharika, ni mwandani wa muda mrefu wa Rais mpya na kwamba alikuwa
sambamba naye katika kampeni za uchaguzi mkuu uliofanyika Mei 20, mwaka
huu na kuhitimisha utawala wa miaka miwili na ushee wa Rais Joyce Banda.
“Baada ya shughuli za kanisani, chereko zitahamia katika familia ya Mutharika iliyopo Ndata katika Wilaya ya Thyolo,” imeeleza sehemu ya taarifa hiyo.
Tukio
la kuoa na kuwasili kwa watoto wake, kumeelezwa kumaliza uvumi uliokuwa
umeenezwa na wapinzani wake kisiasa kuwa, Mutharika hakuwa mwanamume
aliyekamilika.
Uvumi
huo ulijibiwa na Katibu Mkuu wa DPP, Chimwemwe Chipungu mara baada ya
kuwapokea mabinti hao kwenye Uwanja wa Ndege wa Lilongwe wakitokea
Marekani, akisema: “Watu walikuwa na hofu kama Rais Mutharika ana
watoto. Ni uvumi wa kijinga. Waliokuwa wakieneza uvumi huo sasa watapata
aibu. Rais wetu ana watoto na ni baba wa familia.”
Na
Rais Mutharika mwenyewe, wakati wa kampeni aliyasigina maneno ya
wapinzani wake kwa kusema ana watoto wenye afya njema, akili timamu na
wanasheria maarufu Marekani, mmoja akiwa Profesa katika moja ya vyuo
vikuu vya huko.
“Ukiachana
na watoto, pia nina wajukuu kadhaa,” alisema Mutharika mwenye umri wa
miaka 74 sasa ambaye akiwa mwanazuoni katika masuala ya sheria, aliwahi
kufundisha katika vyuo kadhaa, kikiwemo Chuo Kikuu cha Dar es Salaam
(UDSM) katika miaka ya 1970.
Kabla
ya kuutwaa urais wa Malawi, Profesa Mutharika aliyebobea katika masuala
ya sheria ambaye pia ni mwanasiasa mzoefu na mashuhuri, ameshika
nyadhifa za uwaziri katika wizara mbalimbali zikiwamo Wizara ya Sheria,
Wizara ya Mambo ya Nje na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, nafasi
aliyoishika hadi anaingia katika uchaguzi mkuu hivi karibuni.
