MAKAMU wa Rais wa Jamhuri ya Watu wa China, Li
Yuanchao, amewasili leo (Jumapili Juni 22, 2014) nchini
kuanza ziara yake ya siku 5 ya Kiserikali hapa nchini.
Akiwa
katika uwanja ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere, Mhe. Yuanchao amepokelewa
na Mwenyeji wake Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.
Mohammed Gharib Bilal na Viongozi mbalimbali wa Serikali.
Kwa
Mujibu wa ratiba iliyotolewa leo Jumapili Juni 22, 2014 na Ofisi ya Intifaki
katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, katika siku yake ya
pili ya ziara yake Jumatatu Juni 23, 2014, Mhe. Yuanchao anatarajia kukutana na
Viongozi wa Serikali akiwemo Rais Jakaya Kikwete, Makamu wa Rais Dkt. Mohammed Gharib
Bilal na Waziri Mkuu Mizengo Pinda Ikulu Jijini Dar Es Salaam.
Aidha
mbali na kukutana na Viongozi hao, Mhe. Yuanchao akiwa na Mwenyeji wake Makamu
wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Mohammed Gharib Bilal pia
anatarajia kufungua mkutano wa Jukwaa la Uwekezaji baina ya Tanzania na China
katika ukumbi wa mikutano wa Benki Kuu
ya Tanzania.
Katika
siku ya tatu ya ziara yake Jumanne (Juni 24, 2014), Mhe. Yuanchao, anatarajia
kukutana na Viongozi wa Chama cha Mapinduzi CCM akiwemo Makamu Mwenyekiti, Bw,
Philip Mangula katika hateli ya Serena na baadaye kuweka jiwe la msingi la
ujenzi wa Ofisi Mpya za Ubalozi wa China hapa nchini.
Mhe.
Yuanchao katika siku ya nne Jumatano (Juni, 25, 2014) ya Ziara yake anataraji
kushiriki katika hafla ya ukataji utepe wa kuzinduliwa kwa vifaa vya kubebea
mizigo mizito katika ofisi za Mamlaka ya Usafiri wa Reli wa Tanzania na Zambia
(TAZARA) na baadae kusafiri na treni kutokea Kituo cha Tazara hadi Yombo
akiongozana na Waziri wa Uchukuzi, Mhe. Harrison Mwakyembe.
Aidha
katika siku hiyo pia, Mhe. Yuanchao anatarajia kukutana na Wawekezaji kutoka
China wanaofanya shughuli zao hapa nchini na baadaye kuelekea Zanzibar ambapo
atakutana na Makamu wa Pili wa Rais Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi pamoja na
Madaktari kutoka China waliopo katika eneo la Vuga.
Aidha
katika siku ya mwisho ya ziara yake hapa nchini Alhamisi (Juni 26, 2014), Mhe.
Yuanchao akiwa Zanzibar anatajia kutembelea eneo la makumbusho la Stone Town na
kujionea makumbusho mbalimbali ya kihistoria ikiwemo Soko la zamani la watumwa. Makamu
huyo wa Rais kabla ya kumaliza ziara yake hapa nchini (Alhamisi Juni 26, 2014) anataraji
kukabidhi gari la kurushia matangazo kwa Kituo cha Televisheni ya Taifa (TBC)
na baadaye jioni kupanda ndege kurejea nyumbani nchini China.
Na Ismail Ngayonga
MAELEZO
Dar es Salaam
22. Juni, 2014
