MAJAMBAZI WAIBA MAMILIONI YA FEDHA KWENYE KITUO CHA KUUZIA MAFUTA MKOANI MWANZA

WATU wanaodhaniwa kuwa majambazi usiku wa kuamkia jana wamevamia kituo cha mafuta Smat Usagara, kilichopo wilayani Misungwi na kuiba kiasi kikubwa cha fedha.

Akizungumzia hilo, mmoja wa watumishi wa kituo hicho, Janet Alex (36), mkazi wa Usagara, amesema kuwa akiwa kazini majira ya usiku wa saa tano, walikuja wateja wakiwa na gari wakihitaji mafuta aina ya petroli lita 200.

Amesema alianza kuwahudumia na zilipofikia lita 156 alivamiwa na kundi la majambazi wapatao 10 wakiwa na silaha na kuwaamuru wateja walale chini huku watatu wakiondoka naye kuelekea ofisini, ambako kulikuwa na sefu ya kutunzia fedha na kumwamuru awapatie fedha.

Amebainisha kuwa majambazi hao waliiona sefu hiyo na kuamua kuilipua kwa kitu kinachodhaniwa kuwa ni baruti na kuisambaratisha na kufanikiwa kuchukua fedha za mauzo ya siku tatu zilizokuwepo.

Janet amesema kuwa mauzo ya siku moja ni kati ya sh milioni 10, hivyo kiasi walichokichukua hakipungui sh milioni 30.

Amebainisha kuwa licha ya kuiba fedha zilizokuwamo kwenye sefu, pia walipora nyingine kwa wateja waliokuwamo kwenye gari lililokuwa likijaza mafuta.

Matukio ya ujambazi yameendelea kushamiri katika Jiji la Mwanza, ikiwemo Wilaya ya Misungwi eneo la Usagara ambapo hivi karibuni majambazi walipora fedha katika kituo hicho pamoja na cha jirani yake, Lake Oil.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Valentino Mlowola, amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kusema kuwa Jeshi la Polisi mkoani Mwanza linawahoji watu watatu kuhusiana na tukio hilo ambapo majina yao hakuwa tayari kuyataja kwa kuwa upelelezi bado unaendelea.

Na  Antony Sollo


JIUNGE NA EDMO BLOG SASA

Usipitwe!! Jiunge nasi kupitia Facebook,Twitter na Instagram ili kupata habari zote za town! Usikose kujiunga na Youtube kuangalia video zote kali kutoka Edmo Blog Pekee!, kujiunga bonyeza hapa>>>Youtube

Tupe Maoni Yako lakini Usiandike Matusi



 
© Copyright EDMO BLOG | Designed By Peruzibongo