HUDUMA DHAIFU KWENYE HOSPITALI, VITUO VYA AFYA NA ZAHANATI VYALALAMIKIWA RUVUMA

WANANCHI mkoani Ruvuma wamelalamikia kitendo cha Hospitali ya Rufaa ya mkoa huo pamoja na vituo vya Afya na Zahanati, kutoa huduma za afya zisizoridhisha na kuwepo kwa vitendo vya kuomba na kupokea rushwa hali ambayo imetajwa kusababisha baadhi yawagonjwa wasio na fedha kukosa matibabu stahiki. 

Wakazi hao wametoa malalamiko hayo wakati wakiongea  Juni 13, 2014 na kusema wamekuwa wakidaiwa kiasi kikubwa cha fedha kwa ajili ya kupatiwa huduma husika na baadhi ya watoa huduma za afya mkoani humo, na pindi wanaposhindwa kutoa fedha kidogo ‘rushwa’ wagonjwa wao hukosa huduma kwa muda mrefu na kuendelea kubaki hospitalini, zahanati na katika vituo vya afya kwa muda mrefu.
 
Kaimu Mkuu wa mkoa wa Ruvuma ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya ya Songea, Joseph Mkirikiti, ameahidi kushughulikia kero hizo ya huduma ya afya pamoja na malalamiko mengine ya wananchi ambayo ameyapata likiwemo suala la mahusiano mabaya baina ya wananchi na Jeshi la Polisi mkoani humo.
 
Amekemea na kupiga marufuku tabia ya viongozi wa siasa wilayani humo, kutumia nafasi ya kuwarubuni wananchi kwa changamoto zinazowakabili katika kipindi cha uchaguzi wa serikali za mitaa unaotarajiwa kufanyika hivi karibuni, kwani kufanya hivyo upo uwezekano wa kuchochea vurugu na machafuko kwa wananchi kudai haki zao kwa nguvu.
 
licha ya Mganga Mkuu Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa mkoani humo, Benedicto Ngaiza, kuwataka wananchi kutokubali kutoa rushwa kwa ajili ya huduma yoyote na pindi wanapodaiwa rushwa watoe taarifa kwa uongozi wowote ili hatua ziweze kuchukuliwa dhidi ya wahusika bado tatizo hilo limeendelea kuota mbawa.
CHANZO:FIKRA PEVU


JIUNGE NA EDMO BLOG SASA

Usipitwe!! Jiunge nasi kupitia Facebook,Twitter na Instagram ili kupata habari zote za town! Usikose kujiunga na Youtube kuangalia video zote kali kutoka Edmo Blog Pekee!, kujiunga bonyeza hapa>>>Youtube

Tupe Maoni Yako lakini Usiandike Matusi



 
© Copyright EDMO BLOG | Designed By Peruzibongo