KATIBU wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM, Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye amesema ‘ndoa’ upinzani bungeni iliyozaa Baraza Kivuli la Mawaziri la vyama vya Chedema, CUF na NCCR-Mageuzi, ni mwendelezo wa ubabaishaji na matusi makubwa kwa vyama vingine vilivyokubali ndoa hiyo hasa CUF.
Nape
amesema hayo jana wakati akihutubia mkutano wa hadhara kwenye viwanja
vya Parking mjini Nzega na kusema kuwa mwenendo huo wa vyama vya
upizani, utasambaratisha na kuua vyama vya upizani nchini.
Akinukuu
taarifa rasmi za Bunge zilizomkariri Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu
Lissu (Chadema), Nape alisema ameshangazwa na pande zote mbili za ndoa
ya Chadema na CUF.
“Ngoja
ninukuu baadhi ya maneno ya kejeli na matusi kutoka kwa Tundu Lissu kwa
vyama vya upizani vilivyopo bungeni ili kuthibitisha unafiki mkubwa wa
wapizani wanchi hii. “Na hili nimeamua kulisema baada ya waandishi wengi
kutaka kujua kauli yangu juu ya Baraza Kivuli la Mawaziri lilitangazwa
na Mbowe (Freeman, Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni) hivi
karibuni,” alisema Nape huku wananchi wa Nzega wakimshangilia kwa makofi na vigelele.
Nape
alisema matusi aliyotukana Lissu bungeni dhidi ya vyama vya upinzani
vyenye wabunge bungeni, hayavumiliki na ni ajabu kuwa pande zote za ndoa
ya vyama vya upinzani bungeni wamesahau.
“Tundu
Lissu alihoji bungeni kuwa inawezekanaje kuunda Kambi moja Rasmi ya
Upinzani bungeni wakati vyama vina Katiba tofauti, kanuni tofauti na
taratibu tofauti za kuendesha mambo yake,” alisema Nape na kuongeza
kuwa inawezakanaje Kiongozi huyu wa Kambi ya Rasmi ya Upinzani bungeni,
akasimamia nidhamu kwa muungano wa namna hii?
“Leo
kimetokea nini kilichombadilisha Lissu na Chama chake kama sio unafiki?
Ni lini walibadili Katiba, Kanuni na taratibu kabla hawajaunda mseto
wao? “Akawakejeli sana CUF na kujiapiza kuwa Chadema haitakubali kuwa na
ndoa na Chama chenye ndoa nyingine… sasa hiyo ndoa ya kwanza imekufa
lini?” Alihoji Nape.
