ALIYEJIFUNGUA PACHA WANNE ANAOMBA MSAADA WAKO

MKAZI wa Kijiji Chakijage, Kata ya Rwabwere, Wilaya ya Kyerwa mkoani Kagera, aliyejifungua watoto wanne pacha, Jodephina Rugambwa (30), ameiomba serikali kumpatia msaada ili kumsaidia kulea watoto wake.

Akizungumza na waandishi wa habari waliomtembelea nyumbani kwake jana, alisema furaha ya kupata watoto wake hao aliojifungua Machi 23, mwaka huu inaanza kutoweka kwa kuwa anashindwa kuwatunza kutokana na kipato duni alichonacho.

“Mimi na mume wangu ni wakulima wadogo wenye kipato kisichoweza kutusaidia kwa wakati huu kuwatunza watoto hawa, hivyo tunaomba msaada wa hali na mali kutoka serikalini na kwa wasamaria wema,” alisema.

Alisema mbali na watoto hao wanne, familia yake imejaliwa watoto wengine watatu ambao wawili wanasoma.

Hata hivyo, mama huyo pamoja na mumewe Donati Anatory (38), wameishukuru Ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kyerwa, wasamaria wema pamoja na wajumbe wa Baraza la Madiwani wilayani humo kwa msaada wao wa hali na mali uliofikia hadi sasa kiasi cha sh 400,000.

Watoto hao pacha, wa kike wakiwa watatu na mvulana mmoja walizaliwa salama wakiwa na afya njema.

Na Ashura Jumapili.


JIUNGE NA EDMO BLOG SASA

Usipitwe!! Jiunge nasi kupitia Facebook,Twitter na Instagram ili kupata habari zote za town! Usikose kujiunga na Youtube kuangalia video zote kali kutoka Edmo Blog Pekee!, kujiunga bonyeza hapa>>>Youtube

Tupe Maoni Yako lakini Usiandike Matusi



 
© Copyright EDMO BLOG | Designed By Peruzibongo