Mkazi wa
Kijiji cha Butengo, wilaya ya Chato, mkoani Geita, Maria Bujingu (42),
ameuawa kinyama na watu wasiojulikana, ambao wametoweka na viungo vyake
mbalimbali vya mwili, zikiwamo sehemu za siri.
Viungo vingine ambavyo wauaji walitoweka navyo ni pua, kidevu, kidole gumba cha mguu wa kulia na nyama za mkono wa kushoto.
Mauaji hayo
ya kikatili yamezua hofu kubwa kutokana na kuwapo mazingira
yanayokanganya, baadhi yakihusishwa na imani za kishirikina na mengine
kisasi.
Kutokana na
hali hiyo, baadhi ya wanakijiji wamekuja juu wakitaka uchunguzi wa kina
ufanyike, ikiwamo baadhi ya viongozi wa kijiji hicho kuhojiwa.
Wanakijiji
hao wanataka uchunguzi huo ufanyike kwa madai kwamba, kabla marehemu
kufikwa na umauti, kulikuwa na mgogoro, ambao unafahamika.
Habari
zilizopatikana kutokana katika kijiji hicho juzi na jana zinadai kuwa
marehemu aliondoka nyumbani saa 3.00 usiku, Aprili 22, mwaka huu, akidai
kwenda kwa mmoja wa jamaa.
Hata hivyo,
habari hizo zinasema baada ya kuondoka, marehemu hakurejea hadi mwili
wake ulipopatikana Aprili 25 mwaka huu, umbali wa kilometa mbili kutoka
nyumbani kwake akiwa ameuawa na kunyofolewa baadhi ya viungo vya mwili
wake.
Mmoja wa
watoto wa marehemu, Jesca John, ndiye alielezea mazingira ya mama yake
kuondoka nyumbani na kisha kutorejea hadi alipopatikana akiwa ameuawa.
Inadaiwa
kuwa wakati huo mume wa marehemu alikuwa kwenye mji wake wa pili katika
Kijiji cha Lumasa na kwamba, kumekuwapo na tetesi za kuwapo mtafaruku
ndani ya ndoa yao.
Kaimu
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Geita, John Temu, alithibitisha kufanyika kwa
mauaji hayo na kwamba, tayari mwanakijiji mmoja alikuwa anashikiliwa
kutokana na tukio hilo. “Ni kweli mwandishi.
Baada ya
kufuatilia kwa OCD (Mkuu wa Polisi Wilaya) wangu wa Chato imethibitika
tukio hilo lipo na tayari mtu mmoja anashikiliwa kuhusiana na tukio
hilo,” alisema Kamanda Temu.
Aliongeza:
“Hata hivyo, tunajaribu kuingia kwa undani kutambua chanzo chake iwapo
ni imani za kishirikina au mhalifu anaweza kutumia tu mwanya huo
kupoteza ukweli kumbe hayatokani na imani za kishirikina.”
Kumewapo na
taarifa za kukanganya katika kijiji hicho, ambazo baadhi zinadai kuwa
mwaka jana kabla ya marehemu kufikwa na mauti, kuna matukio ambayo
yaliashiria hali ya hatari kwake, lakini hakuna hatua zilizochukuliwa
kuweka mambo sawa.
Inadaiwa
kuwa mwaka jana marehemu alikuwa kati ya wanawake watano waliofukuzwa
katika kijiji hicho hadharani na viongozi wa kijiji kwenye mkutano
ulioongozwa na viongozi wa ulinzi wa jadi sungusungu wa kijiji hicho.
Kwa mujibu wa habari hizo, wanawake hao walifukuzwa katika mkutano huo baada ya kutuhumiwa kuwa ni wachawi.
Hata hivyo, inadaiwa kuwa tuhuma hizo zilipandikizwa na kuunga mkono na baadhi ya viongozi kutokana na chuki binafsi.
Uchunguzi
wa kina uliofanyika katika kijiji hicho, umebaini kuwa marehemu na
wanawake wengine waliotambuliwa kwa majina ya Bertha Musa, Bhati
William, Ndebile Nyanda na Sweka Zacharia, walifukuzwa katika kijiji
hicho.
Hata
hivyo, baada ya malalamiko hayo kuifikia ofisi ya mkuu wa wilaya ya
Chato na polisi, baadhi ya viongozi walikamatwa na kuamriwa kuwaruhusu
wanawake hao, akiwamo marehemu kurejea katika kijiji hicho.
Hata hivyo,
habari hizo zinasema kuwa hadi kufikia juzi, mmoja wanawake hao, Bahati
William alikuwa hajarejea kijijni hapo kutokana na kile kinachodaiwa ni
vitisho kutoka kwa baadhi ya viongozi wanaotuhumiwa kushirikiana na
wanaotuhumiwa kuwafukuza kijijini hapo.
Hali hiyo inadaiwa kuibua mkanganyiko mkubwa juu ya kifo hicho.
Awali, Ofisa
Mtendaji wa Kijiji hicho, Pastory Bugolo, katika mahojiano na mwandishi
wa habari hizi juzi kwa njia ya simu, alithibitisha kuwapo kwa tukio
hilo.
Pia alithibitisha kuwa marehemu alikuwa miongoni mwa wanawake waliokuwa wamefukuzwa kijijini hapo wakituhumiwa kuwa ni wachawi.
Katika tukio
jingine, wanakijiji wengine wanane wakazi wa kijiji cha Mwendakulima,
Kata ya Buetengo-Lumasa, wilayani humo, wakiwamo wanawake, mwaka jana
walifukuzwa kijijini hapo na baadhi ya viongozi wa kijiji hadharani
wakituhumiwa kuwa ni wachawi.
Hatua
hivyo inadaiwa kuyaweka hatarini maisha ya watuhumiwa na baadhi yao
wanadai kuendelea kupewa vitisho na kwamba imekuwa vigumu kusikilizwa
malalamiko yao kutokana na baadhi ya viongozi kuhusika.
Via>> Nipashe
