Mahakama ya Hakimu Mkazi Wilaya ya Chunya mwishoni mwa wiki
iliwahukumu watu tisa kwenda jela jumla kwa miaka 270 baada ya
kupatikana na hatia ya wizi wa kutumia silaha.
Washtakiwa hao ni Samweli Sarehe (40), Bahati
Kenson (29), Aulesi Andason (28) na Ayubu Swila (24), wote wakazi wa
Mbalizi Wilaya ya Mbeya Vijijini.
Wengine ni Mathias Simfukwe (31), Pascal Simchimba
(27) wote wakazi wa Kijiji cha Kanga Wilaya ya Chunya, Tegemea Kenya
(27) mkazi wa Kijiji cha Mjele, Shukuru Mwakatumbula (27) wa Ifumbo na
Maleba Kindagilo (46) wa Lupa, Chunya.
Awali, ilielezwa mahakamani hapo na mwendesha
mashtaka wa polisi, Raymond Lukomwa kuwa washtakiwa wote kwa pamoja
walifikishwa mahakamani hapo Desemba 27, 2013 kwa kosa moja la wizi wa
kutumia silaha kinyume na Kifungu cha 287A cha Sheria ya Adhabu, Sura
ya 16 iliyofanyiwa marekebisho 2012.
Alidai kuwa washtakiwa walifanya kosa hilo Desemba
14, 2013 katika eneo la Kasangakanyika ambako waliiba vipimo vitano vya
dhahabu vyenye thamani ya Sh58 milioni na fedha tasilimu Sh6milioni,
mali ya Paul Sinjale (44) na kwamba katika wizi huo walitumia bunduki
aina ya shortgun.
Akisoma hukumu hiyo, Hakimu Mkazi wa Wilaya ya
Chunya, Desdeli Magezi alisema kwa mujibu wa Kifungu cha Tano (A) (ii)
cha Sheria ya Adhabu, Sura ya 90 iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2002
wote kwa pamoja wanahukumiwa kifungo cha miaka 270 na kila mmoja
atatumikia kifungo cha miaka 30 jela.
