KESI
ya madai iliyofunguliwa na aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu wa Chadema,
Kabwe Zitto dhidi ya chama hicho, imeahirishwa hadi Mei 29 mwaka huu,
itakapotajwa katika Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam.
Msajili wa Mahakama Kuu, Amir Msumi aliahirisha kesi hiyo jana kwa kuwa Jaji John Utamwa anayeisikiliza, anaumwa.
Katika
kesi hiyo, Zitto anaomba Mahakama itoe zuio kwa Kamati Kuu au chombo
chochote cha chama, kujadili uanachama wake hadi atakapokata rufaa ya
kupinga uamuzi uliomvua uongozi wa chama. Anaomba Mahakama imwamuru
Katibu Mkuu, Dk Willbrod Slaa.
Ampe
nakala zinazotoa sababu za uamuzi wa kumvua uongozi katika kikao
kilichofanyika Novemba 22 mwaka jana, ili akate rufaa katika Baraza Kuu
la Chama.
Aidha, anaomba mahakama iamuru Chadema isiingilie kazi zake za ubunge wala uanachama wake.
Zitto
amefungua kesi hiyo dhidi ya Baraza la Wadhamini la chama hicho na Dk
Slaa. Kabla kesi hiyo haijaanza kusikilizwa, Mahakama ilitoa amri kwa
Kamati Kuu au chombo chochote cha Chadema, kutojadili uanachama wa Zitto
hadi kesi hiyo itakaposikilizwa na kutolewa uamuzi.
Katika
uamuzi huo, mahakama ilikubali ombi la Zitto, ambaye ni Mbunge wa
Kigoma Kaskazini, kwa kuwa hoja zake zimekidhi matakwa ya kisheria ya
kutolewa kwa zuio la muda la kujadiliwa kwa uanachama wake.
Jaji
Utamwa alisema Zitto amekidhi matakwa ya kisheria, kwa kuwa zuio hilo
lisipotolewa na akavuliwa uanachama, atapoteza nafasi ya ubunge na
kushindwa kutumikia wananchi waliomchagua na pia atapoteza nafasi ya
Mwenyekiti wa Bunge wa Kamati ya Kudumu ya Hesabu za Serikali.
Zitto
alivuliwa wadhifa wake Chadema, sambamba na aliyekuwa mjumbe wa Kamati
Kuu, Dk Kitilla Mkumbo na Mwenyekiti wa Mkoa wa Arusha, Samson Mwigamba,
kwa kilichodaiwa ni usaliti kwa chama hicho.