MWANAMKE mjamzito anauguza majeraha
katika Hospitali ya Meru Level Five baada ya kudaiwa mumewe aliingiza
chupa kwenye sehemu zake za siri wakati wa likizo ya Pasaka.
Mama huyo
mwenye umri wa miaka 31 alisemekana kupigwa na mumewe, ambaye anahudumu
kama Konstebo katika kambi ya polisi wa utawala ya Gatimbi, Kaunti
ndogo ya Imenti.
Akieleza masaibu yake
akiwa hospitalini, mama huyo alisema mumewe aliyekuwa mlevi aliwasili
nyumbani mwendo wa saa tisa alfajiri Jumamosi na kumwagiza avue nguo
zote akiwa nje.
Alisema
alitii maagizo hayo na polisi huyo akavaa sare yake ya kazi, akachukua
chuma na risasi mbili kisha kumpiga na kusema kwa sauti kuwa ataua mtu
siku hiyo.
Mshukiwa alimwambia arudi nyumbani ambapo aliwasha runinga ili mkewe asisikike akipiga nduru ambazo zingeamsha majirani.
“Hapo ndipo
alipochukua chupa ya pombe aliyokuwa amebeba na chuma, akaziingiza
kwenye sehemu zangu za siri. Alinifunika mdomo ili nisipige kelele,”
alieleza huku akidondokwa na machozi.
Alizimia kwa saa kadha ndani ya nyumba huku akivuja damu nyingi.
“Niliamka
mwendo wa saa 11.30 na kumpata akiwa amelala kitandani, pengine
alizidiwa na pombe nyingi aliyokunywa. Nilitambaa hadi makao makuu ya
kambi ambapo maafisa wengine walinikimbiza hadi hospitalini,” alisema.
Baadaye alilazwa katika zahanati ya Gatimbi ingawa alihamishwa hadi hospitali ya Meru baadaye ili kupokea matibabu maalum.
Kulingana na
Dkt Jamal Mohamed ambaye ni daktari katika hospitali hiyo, hayuko
taabani kwa sasa ingawa bado anahitaji kutazamwa kwa makini.
Mfadhaiko
“Tunamtibu pia kutokana na matatizo ya kiakili aliyopata ingawa anaendelea vyema,” alisema.
Akithibitisha
mkasa huo, Kamanda wa polisi wa utawala katika Kaunti ya Meru, Bw Njue
Njagi, ambaye alimtembelea hospitalini alisema huenda wawili hao
walikuwa na ugomvi wa kinyumbani kabla tukio hilo kutendeka.
Alisema mshukiwa huyo ambaye hakuwa amekamatwa wakati huo, atashtakiwa baada ya polisi kukamilisha uchunguzi wao.
Bw Njagi
alisema afisa huyo ameagizwa kufika afisini na kuongeza agizo la
kukamatwa kwake litatolewa ikibainika alikuwa na hatia.
“Hatujatambua
kilichotokea kabla tukio hilo lakini uchunguzi unaendelea kulihusu.
Atashtakiwa mahakamani ikiwa atapatikana na hatia,” alisema.
Mkuu huyo wa polisi aliomba maafisa wawe wakitafuta ushauri ili kuzuia matukio kama hayo kushuhudiwa.
