Na Ibrahim Yassin ,aliyekuwa Ludewa
Wananchi wa
kata
zilizopo Liuli, Lupingu, Lumbila, Lifuma, Iwela na Kilondo zilizopo Tarafa
ya Mwambao wilayani Ludewa mkoa mpya wa Njombe wameilalamikia
Serikali kupitia halmashauri ya wilaya hiyo kwa kushindwa kuwaondolea
kero
zilizopo katika tarafa hiyo tangu nchi ipate uhuru mwaka 1961 hadi sasa.
Wakizungumza kwa yakati tofauti
wananchi hao walisema kuwa vijiji vilivyopo kwenye kata hizo
vinakabiriwa na changamoto nyingi lakini viongozi wa serikali na halmashauri
wameshindwa kuondoa changamoto hizo kwa muda mrefu na kuwa wamepeleka
malalamiko yao kwa maandishi juu ya matatizo ya Tarafa hiyo lakini hakuna
kinachoendelea.
Dadi mapunda mkazi wa kijiji cha Liunji alisema kuwa Tarafa
hiyo ya mwambao inakabiliwa na changamoto kadhaa ikiwemo ya ukosefu wa umeme, maji
safi, mawasiliano, barabara, shule, vituo vya afya na uhaba wa watumishi ambao
wengi wao hutoroka kufanya kazi mara baada ya kuripoti kutokana na miundombinu
mibovu pamoja na ukosefu wa huduma za msingi za kijamii.
Alisema kuwa katika suala la mawasiliano wamekuwa wakipanda
juu ya miti na kupanda kwenye mirima mirefu huku wengine wakitembea umbali
mrefu kufuata huduma za network hali ambayo inahatarisha maisha yao na kuwa
watoto wao pia hutembea umbali mrefu kwenda shule kutokana na kuwa na shule
chache huku elimu katika Tarafa hiyo ikizidi kushuka siku hadi siku.
Nyongo Makwaya mkazi wa kijiji cha Ndowa kwa upande wake
alisema kuwa Tarafa hiyo ya mwambao imekosa huduma za vituo vya afya vilivyopo
havikidhi mahitaji ya wananchi hali inayopelekea watembee umbali mrefu wa
kutumia Boti na Mitumbwi kufuata huduma za matibabu katika hospitali ya misheni
ya Matema beach na kusababisha baadhi ya wagonjwa kufia njiani kabla hawajafika
hospitali kutokana na umbali mrefu.
Alisema kuwa walikwisha andika barua kuiomba halmashauri juu
ya kero hizo ili iweze kutafuta tiba ya kutatua tatizo hilo lakini bado hali ni
tata na kuwa kama hali itaendelea kuwa hivyo kunauwezekano wa vijana wote ambao
ndiyo nguvu kazi ya vijiji hivyo kuyatelekeza makazi hayo na kwenda kuishi
sehemu nyingine ambako hakuna changamoto kwa lengo la kutafuta unafuu wa
maisha.
Baadhi ya viongozi katika Tarafa hiyo wakiongozwa na Sosten
Haule,Chrispin Mwendapole mbali na kukiri kuwepo na tatizo hilo pia walisema
kuwa serikali kupitia halmashauri ya wilaya ya Ludewa wanalijua tatizo hilo na
wanajipanga ili kujalibu kupunguza changamoto zilizopo.
