RAIS Jakaya Kikwete amesema kama mchakato wa upatikanaji Katiba Mpya utakwama kwa namna yoyote, Katiba iliyopo sasa itafanyiwa marekebisho na kuendelea kutumika.
Alisema
kama Kiongozi Mkuu wa Serikali ni wajibu wake kuwaeleza ukweli wananchi
kama alivyowasilisha hotuba yake kwa wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba
Mjini Dodoma, kuhusu hatari ya muundo wa Serikali tatu ambayo ndiyo
iliyopendekezwa kwenye rasimu.
Rais
Kikwete aliyasema hayo juzi wakati akijibu risala ya wazee wa Wilaya ya
Muheza, mkoani Tanga, waliofanya mazungumzo naye nyumbani kwa Mkuu wa
Wilaya hiyo, Subira Mgalu, akiwa kwenye ziara ya kikazi mkoani humo.
Alisema
Katiba ni jambo muhimu katika nchi na itatumika kwa miaka 50 ijayo
hivyo ni wajibu wa wajumbe kupitisha Katiba bora ambayo utekelezwaji
wake hautakwama baada ya kupitishwa.
Aliongeza
kuwa, pamoja na kasoro zilizopo kwenye Rasimu ya Pili ya Katiba, bado
hakuwasemea wajumbe wa Bunge hilo katika hotuba yake aliyoitoa bungeni
bali aliamua kuweka bayana kasoro husika ili wajumbe waamue wenyewe
muundo wa Serikali mbili au tatu kwani uamuzi ni wao.
"Mimi
niliamua kutoa maoni yangu baada ya kuona Rasimu ina kasoro kwenye
muundo wa Serikali tatu, sikuchukua mamlaka ya wajumbe wa Bunge hili au
kuwaongoza, bali nilieleza kile ninachoamini kinaweza kutupa Katiba
bora.
"Katiba
si kwa ajili ya matumizi ya leo tu, bali kwa vizazi na vizazi, tusije
kutengeneza Katiba ambayo haitekelezeki, lakini wenye maamuzi ni wajumbe
wenyewe, mimi siwezi kuwatolea uamuzi lakini kama Katiba Mpya
itashindwa kupatikana, hii iliyopo itafanyiwa marekebisho na mambo
yataenda," alisema.
Akisoma
risala ya wazee hao, Katibu wao Bw. Hamis Mzee, alisema wao kama wazee
wanaunga mkono hotuba aliyoitoa kwa wajumbe wa Bunge hilo kwani imelenga
kuwahurumia Watanzania na mzigo wanaotaka kubebeshwa na watu wachache.
"Sisi
tunaunga mkono hatuba yako, msimamo wetu ni Serikali mbili ambazo ndizo
zenye uwezo wa kuwahudumia wananchi vizuri si Serikali tatu," alisema
Bw. Mzee.
Awali
Mwenyekiti wa wazee hao, Dorothy Kihampa alisema Rais Kikwete amekuwa
akiwapenda wazee na wao wanamuombea kama alivyoanza salama, basi
atamaliza salama uongozi wake.
Msimamo Baraza la vyama
Wakati
huo huo, Baraza la Vyama vya Siasa, jana limetoa tamko kuhusu mwenendo
wa Bunge Maalumu la Katiba na kusisitiza hauridhishi kama ilivyotarajiwa
na watu wengi.
Akizungumza
na waandishi wa habari Mjini Dodoma jana, Mwenyekiti wa baraza hilo,
Bw. Peter Mziray alisema hali hiyo inatokana na migongano mingi
inayotokea ikiongozwa na makundi ya vyama vya siasa na wanasiasa kwa
nyadhifa zao tofauti.
"Tumekuwa
tukifuatilia na kuangalia kwa makini mchakato huu na kuona wanasiasa
kama wadau wakubwa wanaweza kuukwamisha kutokana na malumbano yasiyo na
tija na mienendo na matendo yasiyokubalika," alisema Bw. Mziray.
Aliongeza
kuwa, wanasiasa wamekuwa wakilalamikiwa katika mchakato huo ambapo
Kamati ya Uongozi ya bara hilo, imebaini uwepo wa makundi yasiyo rasmi
ndani ya Bunge hilo.
"Mfano
wa makundi haya ni UKAWA na Tanzania Kwanza, inaonesha Bunge hili
linayatambua makundi haya ambayo kimsingi kutambulika kwake, kunachochea
mgawanyiko, kujenga uhasama kati ya wajumbe hivyo kudhoofisha dhana ya
kufanya kazi pamoja na kufikia maridhiano.
"Tunatoa
wito kwa wajumbe wote wa Bunge hili, kuacha kujihusisha na makundi haya
badala yake wachambue na kuunga mkono hoja kwa uzito wa hoja yenyewe na
kuzingatia maslahi ya Taifa badala ya kuzingatia mtazamo au msimamo wa
kundi fulani," alisema Bw. Mziray.
Aliwataka
wananchi kutambua kuwa, Bunge hilo ndio nyenzo muhimu ya kupata Katiba
Mpya wanayoitaka hivyo ni vyema wakashiriki kuwahimiza wawakilishi wao
watekeleze majukumu yao vizuri kwa kuepuka kufanya vitendo vya aibu na
kuacha kujali masilahi binafsi bali watangulize utaifa.
"Kamati
hii inasikitishwa na ukosefu wa nidhamu ndani ya Bunge hili jambo
ambalo halikubaliki hata kwa watoto wa shule ya msingi wawapo darasani,"
alisema.
Alitoa
wito kwa wajumbe wa Bunge hilo kuzingatia kanuni ambazo zinakataza
vitendo vyovyote vya utovu wa nidhamu pamoja na kuzomea bali kila mjumbe
anaweza kutoa hoja na inaweza kupingwa au kukubaliwa bila kuzomea.
Bw.
Mziray alisema, kutokana na mwenendo wa Bunge hilo ni vyema Kamati ya
Uongozi wa baraza hilo, ikutane na viongozi wote wakuu wa vyama vya
siasa ambao si wajumbe wa baraza ili kushauriana na kuokoa mchakato huo.
Mbowe atoa lawama
Katibu
wa Kundi la Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA), ambaye ni mjumbe wa
Bunge hilo, Bw. Freeman Mbowe, ameitupia lawala sekretarieti ya Bunge
Maalumu la Katiba akidai inaonekana kupokea maelekezo kutoka serikalini
juu ya uendeshaji wa Bunge likiwemo suala la kubadilisha kanuni za Bunge
hilo.
Bw.
Mbowe aliyasema hayo juzi wakati akizungumza na waandishi wa habari
kuhusu ubadilishwaji wa kanuni na kuongeza kuwa, suala la kubadilisha
kanuni bila ridhaa ya wajumbe ni kutengua azimio la Bunge hilo ambalo
ndilo linalopitisha kanuni hizo.
Alisema
kitendo hicho kinaashiria kutaka kulivuruga Bunge hilo ili mchakato wa
kupata Katiba Mpya usifanikiwe kwani kanuni hizo zilitungwa kwa kipindi
kirefu kupitia semina isipokuwa kanuni ya 37 na 38 inayoeleza aina ya
upigaji kura.
"Aliyepewa
jukumu la kubadilisha kanuni hizi ni nani, inaonekana Sekretarieti ya
Bunge hili inapata maelekezo kutoka nje ya Bunge kwa maana ya
serikalini, wanakaa na kuamua mambo ya Bunge hili na kutuletea, sisi
UKAWA tunataka haki itendeke, hatimae kupata Katiba Mpya kwa maslahi ya
wananchi," alisema.
Aliongeza
kuwa, suala la mabadiliko ya kanuni ni jambo la msingi kwa kila mjumbe
kwani wakati wa kuzipitisha kulikuwa na vikao vya mashauriano miongoni
mwa pande mbili zilizokuwa zikivutana katika suala hilo hivyo kitendo
cha kuzifungua kanuni hizo ni mkakati wa makusudi wenye kutaka kuleta
chuki bungeni.
Kwa
upande wake, Profesa Ibrahim Lipumba alizungumzia hotuba ya Rasi Jakaya
Kikwete na kusema, imesikitisha kwani hakuona umuhimu wa masuala ya
Muungano na haki za wanawake.
Alisema
Rais Kikwete alipaswa kulizindua Bunge hilo kwa kuwataka wajumbe kutoa
maoni yao juu ya Rasimu ya Pili ili baadaye maoni hayo yapelekwe kwa
wananchi lakini Rais alivunja kanuni za Bunge kwa kuhutubia masilahi ya
CCM.
Prof.
Lipumba aliongeza kuwa, UKAWA hawapo tayari kuondoka katika Bunge hilo
na kuwaacha wajumbe wa CCM waandike Katiba yao kwani watakuwa
wamewaangusha wananchi wanaowawakilisha ili kupata Katiba bora.
>>Majira
>>Majira