Mwanamke aliyetajwa kwa jina la Jessica Dutro, anakabiriwa na kesi ya mauaji huko Washington Marekani baada ya kutuhumiwa kuwa alimpiga mwanae wa miaka 4 hadi kumuua baada ya kuhisi kuwa atakuwa ‘shoga’.
Waendesha mashitaka walidai kuwa August 14, 2012 mama huyo aliwapiga
vibaya watoto wake watatu, lakini kipigo kilikuwa kikali zaidi kwa
mwanae aitwae Zachary Dutro- Boggess ambaye alimuudhi zaidi baada kuona
kuwa anatabia za kishoga mapema akiwa mtoto.
Baada ya kipigo kikali mtoto huyo alipelekwa hospitalini siku hiyo na
kitengo cha dharura na kuwekwa kwenye mashine ya kumsaidia kupumua,
hata hivyo baada ya siku mbili alipoteza maisha.
Ushahidi uliofikishwa mahakamani mwanzoni mwa mwezi huu na muendesha
mashitaka, Megan Johnson unaonesha kuwa ujumbe wa Facebook aliotuma
mwanamke huyo kwenda kwa mpenzi wake aitwae Brian Canady ndio uliobeba
sababu ya chanzo cha kichapo kikali alichopewa mtoto huyo.
Alimueleza kuwa mtoto wake anaelekea kuwa shoga.
“Anatembea na kuongea kama vile (shoga). Ugh.” Ilisomeka sehemu ya
ujumbe huo uliokuwa ukimueleza mpenzi wake huyo kuwa anampiga mwanae
muda huo.
Kutokana na majibishano ya kwenye Facebook, mpenzi wake huyo pia
alifunguliwa mashitaka na mahakama ikamkuta na hatia mwanzoni mwa mwezi
huu kwa mchango wake kufuatia kifo cha mtoto huyo, kwa kuwa ujumbe mmoja
ulionesha kuwa mwanamke huyo alimpa jukumu la kumfanyia kazi mtoto
huyo.