Suala la utoro kwa wanafunzi waliochaguliwa kuanza kidato cha kwanza Januari mwaka huu, pamoja na wale waioanza kidato cha kwanza na kutoroka njiani bila kufuka kidato cha nne, vimeonesha kumchefua mkuu wa mkoa wa Njombe kapteni mstaafu Aseri Msangi (pichani) wakati akiendelea na ziara yake wilayani Makete
Hali hiyo imemfanya mkuu huyo wa mkoa kutoa agizo la kuhakikisha wanafunzi wote waliochaguliwa kuingia kidato cha kwanza mwaka huu na miaka iliyotangulia wanakuwepo shuleni na ikibidi nguvu ya ziada (vyombo vya dola) vitumike kuhakikisha wanafunzi hao wanarudi shuleni
Akizungumza kwenye ziara yake aliyoifanya Mang'oto sekondari Kapteni Msangi amesema inashangaza kuona wanafunzi waliotakiwa wawepo darasani hawapo na hakuna sababu za msingi zilizosababisha wanafunzi hao watoroke, hivyo kutaka wanafunzi hao watafutwe na warejeshwe shuleni mara moja
"Hivi tunataka kutengeneza taifa la aina gani, kama watoto wanatoroka na ninyi mnakaa kimya, wazazi na walezi nao wanakaa kimya, hatukubali kuwa na taifa la watu wajinga, naagiza wanafunzi waliotoroka wote warejeshwe shuleni mara moja" alisema Msangi
Akisomewa taarifa ya shule na mkuu wa shule Mwalimu Mgaya, taarifa hiyo imeeleza shule hiyo kukosa maabara jambo lililomshangaza mkuu wa mkoa kwa kuwa wapo wanafunzi wa naosoma masomo ya sayansi na wanasoma nadharia tu bila vitendo

Akiwa katika ukaguzi wake ameshauri vyumba 5 vya madarasa ambavyo kwa sasa havitumiki vitumike kama maabara badala ya kuanza kujenga upya majengo mapya kwa kuwa muda unakwenda na agizo alilolitoa rais kuwa kila shule iwe na maabara kufikia Novemba mwaka huu, huwenda likachelewa
"Nashauri, vyumba hivi vitatu au vile viwili vitumike kama maabara, kwa sasa muumize kichwa kuvifanyia ukarabati humu ndani wa namna itakavyokuwa maabara na si vinginevyo badala ya kuendelea na mpango wenu wa kujenga maabatra mpya ili hali vyumba hivi vina kaaa tu" alisema Msangi
Mkuu wa mkoa yupo wilayani Makete kwa ziara ya kikazi ya siku 3.