FAMILIA ya Baba wa Taifa, Mwalimu Julius
Nyerere, imeporwa kiwanja ilichokuwa inamiliki na anayedaiwa kuwa
mporaji ameanza ujenzi ambao unafanyika chini ya usimamizi wa walinzi wa
miraba minne.
Mtoa habari kutoka familia hiyo (jina limehifadhiwa),
amesema kiwanja kilichoporwa kiko Msasani Beach karibu na makazi ya
mjane wa Mwalimu, Mama Maria na ni namba 778.
Mtoa habari huyo ambaye alifika katika
ofisi za gazeti hili, alibainisha kuwa waporaji hao wameonesha kiburi
kiasi cha kukaidi agizo la Polisi la kuwataka waache kuendelea na ujenzi
katika eneo hilo mpaka litakapopatiwa ufumbuzi.
Uporaji Kutokana na taarifa hizo, gazeti
hili lilitembelea nyumbani kwa Mwalimu kuthibitisha taarifa hizo na
kukutana na mwanafamilia mwingine, ambaye ni mkwe wa Mwalimu.
Mkwe huyo wa Mwalimu alimtaja mmoja wa
wavamizi hao (jina limehifadhiwa) na amekuwa akidai kuuziwa kiwanja
hicho na mtoto wa Mwalimu.
"Huyo mtoto wanayesema amewauzia hicho
kiwanja anaumwa, hata kisheria haruhusiwi kuingia mkataba kwa hiyo
tunarudi pale pale kuwa ni matapeli tu hawana jingine lolote," alisema.
Baada ya kuvamia kiwanja hicho, mtoa
habari alisema waporaji hao wamefanya ujanja na kukigawa viwili; kimoja
kina namba 778 na kingine 782, wakati awali kilikuwa na namba moja 778.
Alidai hata nyaraka wanazodai kuuziana na mtoto huyo wa Mwalimu
zimeghushiwa, kwa kuwa mtoto mwenyewe alipoulizwa, alikana kuuza kiwanja
hicho na kuongeza kuwa hata saini inayoonekana katika nyaraka hizo si
yake. Mwalimu ni nani?
Katika kuonesha kiburi cha waporaji
wanaodaiwa kuwa wafanyabiashara, mtoa habari huyo alisema wamekuwa
wakitamba kuwa hakuna mtu wa kuwafanya chochote huku wakihoji Mwalimu ni
nani?
"Wanatamba hakuna mtu anayeweza kufanya
chochote...wanafikia hatua ya kuhoji Nyerere ni nani, eti alikuwa
zamani, lakini kwa sasa hana chochote. Hizi kashfa zinatukera," alisema.
Alisema pamoja na kukerwa na hali hiyo, wameamua kuacha suala hilo kwa
vyombo husika, ili vichukue hatua na wamemteua wakili awasaidie.
"Sisi tunashindwa kuelewa, kwa sababu
anafanya vile anavyotaka. Kuna kipindi alianza kumwaga kifusi, tukaenda
kwa OCD (Mkuu wa Polisi wa Wilaya), akaja akamwambia aache kuendelea
kumwaga kifusi,” alisema.
Alisema pamoja na agizo hilo la OCD,
mfanyabiashara huyo ameendelea kumwaga kifusi katika eneo hilo ili
kuanza ujenzi na shughuli hiyo hufanyika usiku chini ya ulinzi wa
mabaunsa hao.
Alibainisha kuwa mkesha wa Januari 22
mwaka huu saa 7 usiku, mtuhumiwa alifika eneo hilo na mabaunsa wapatao
30 ambao walikuwa wakirandaranda, ili kusimamia umwagaji kifusi na
kusawazisha, huku mmoja wa waporaji hao (jina tunalo) akiwa ameshikilia
bastola.
Wakili wa familia hiyo aliyejitambulisha
kwa jina moja la Banzi, alipozungumza na gazeti hili, alisema alipata
taarifa za uvamizi wa Jumanne usiku lakini hajachukua hatua za kisheria.
Alisema alichelea kuchukua hatua za
kisheria, kwa kuwa alikuwa na ahadi ya kukutana na Mkuu wa Wilaya ya
Kinondoni, Jordan Rugimbana, hivyo alikuwa akisubiri aone suala hilo
litakapofikia na kama ikishindikana, achukue hatua zaidi.
"Niko na familia kwa karibu katika suala
hili, haya ni mambo ya kusikitisha hata kibinadamu, haiwezekani familia
ya muasisi wa Taifa hili inafanyiwa mambo kama haya," alisema Banzi.
DC akiri, ashituka Rugimbana alipoulizwa
kuhusu suala hilo, alikiri kufikishwa ofisini kwake na tayari ameanza
kulishughulikia kwa kuamuru Manispaa ya Kinondoni kumpelekea nyaraka
zote zinazohusu kiwanja hicho.
"Watu wa Manispaa wameniomba niwape muda
ili wafuatilie suala hilo huko Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya
Makazi, lakini tayari tumekutana na upande wa walalamikaji na sasa
tunasubiri kukutana na upande unaolalamikiwa," alisema Rugimbana.
Alisema wanachotaka kujiridhisha, ni
kama kweli huyo mtu ameuziwa kiwanja hicho na mtoto huyo. "Kwa kweli
mambo yaliyoko pale ni ya kisheria zaidi ndiyo maana nataka kutumia
vyombo vyote ili tujiridhishe."
Alipoulizwa kama watu hao wanaendelea na
ujenzi huo, Rugimbana alisema kupitia Polisi Mkoa wa Kinondoni,
wamemwamuru mdaiwa huyo asimamishe ujenzi hadi suala hilo litakapopata
ufumbuzi.
"Hilo la kuendelea na ujenzi sina
taarifa nalo, kwa kuwa pamoja na mtu huyo kudai eneo hilo ni lake,
lakini tumemsimamisha ujenzi ... hiyo haraka ya kujenga inatoka wapi?”
alihoji Rugimbana na kusisitiza kuwa atafuatilia kuona kama kweli ujenzi
huo unaendelea.
Alisema lengo la kumsimamisha mtuhumiwa
ni kutoa fursa kwa Manispaa kutafuta na kuwasilisha kwake vielelezo
vyote vya eneo hilo. Alisema atatoa ufafanuzi zaidi suala hilo
litakapopatiwa ufumbuzi na ofisi yake
CHANZO:HABARILEO
