MARAFIKI wa mwanamume ambaye alikuwa amedaiwa kufariki walipigwa na butwaa na kutoroka baada ya mwanamume huyo kugunduliwa kuwa alikuwa hai katika ufuo wa Machakos Level Five leo adhuhuri.
Polisi
walikuwa wamepata mwili wa mchuuzi huyo anayedaiwa kuwa wa umri wa miaka
45 katika mtaro kwenye kituo cha mabasi cha Machakos.
Walifululiza hadi
kwenye mochari wakiandamana na marafiki zake lakini wahudumu
walipouchunguza ‘mwili’ wakagundua kwamba mchuuzi huyo alikuwa anapumua.
Wahudumu hao
walimkimbiza hadi kwenye wodi iliyo karibu na akawekwa mirefeji ya
kupumua, kupewa dawa na kuongezwa maji mwilini. Madaktari walisema
alikuwa amedhoofika kiasi kwamba hangeweza kupata tena fahamu. Baadaye
alifariki mwendo wa saa nane.
Marafiki zake
walijawa na huzuni mwili wa mchuuzi huyo ulipokuwa ukipelekwa kwenye
mochari mara ya pili. Jina la mwanamume huyo halikutolewa, huku
madaktari wakisema wanasubiri jamaa zake wafahamishwe rasmi kuhusu kifo
chake.
Marafiki zake
waliohojiwa na KNA walisema marehemu alipokuwa hai alikuwa amelalamika
kwamba alikuwa anahisi maumivu makali kifuani. Walisema mchuuzi huyo
alikuwa ameonywa dhidi ya kunywa pombe kupindukia kwa sababu alikuwa na
matatizo ya kiafya.
Walisema alikuwa amelala mtaroni kwa zaidi ya masaa sita baada ya kunywa pombe.