
Kufuatia kuwepo hatari ya kukatika mawasiliano ya barabara ya Makete-Bulongwa-Mbeya kufuatia kumeguka kwa kingo za barabara karibu na daraja la Ilolo wilayani Makete mkoani Njombe kufuatia mvua zinazoendelea kunyesha wilayani hapo, wahusika wametakiwa kulichukulia uzito suala hilo
Mtandao huu umeshuhudia hatari ya kumeguka kwa barabara katika eneo hilo hali ambayo endapo haitachukuliwa hatua za haraka itasababisha barabara hiyo kukatika na kutopitika kabisa
Kufuatia hatari hiyo, mwandishi wa mtandao huu alibisha hodi ofisini kwa mkuu wa wilaya ya Makete mh Josephine Matiro ambaye alikiri kupata taarifa za tukio hilo ambapo aliwasiliana kwa njia ya simu na meneja wa TANROADS mkoa wa Njombe ambao waliahidi kufika mara moja kwenye eneo hilo
Mh. Matiro amesema anatambua adha ambayo wakazi wa makete wataipata endapo eneo hilo litakatika na kuahidi kuendelea kulisimamia ipasavyo suala hilo hadi litakapomalizika ili kuondoa usumbufu utakaojitokeza
Mwandishi wa mtandao huu amefika eneo hilo na kukuta hatua za awali zilizochukuliwa na TANROADS mkoa wa Njombe ambao kama walivyosema watafika mara moja ni kweli walifika na kuzungushia alama za tahadhari eneo hilo huku wakiendelea na hatua zaidi za kukarabati eneo hilo