KUNDI la Jahazi Modern Taarab limefafanua ni
kwanini limeamua kuuchagua mji wa Morogoro kama kituo chao cha kwanza cha
kutambulishia nyimbo zao mpya zitakazounda albam yao mpya ijayo.
Jahazi wanatagemewa kufanya onyesho maalum
Morogoro kwaajili ya kuwaonyesha nyimbo mpya mashabiki wao Ijumaa ya tarehe 31
mwezi huu ndani ya ukumbi wa Tanzanite Complex.
Jana kiongozi wa Jahazi Modern Taraab Mohamed
Mauji alifanya mahojiano na kipindi cha Sham Sham za Pwani cha ITV
kinachoongozwa na mtangazaji Hawa Hassan (Kama wanavyoonekana pichani) ambapo
msanii huyo alitoa sababu kadhaa ni kwanini wameichagua Morogoro. Kipindi hicho
kitaruka hewani Jumamosi hii saa 11 jioni.
Mauji ambaye ni mcharazaji gitaa la solo
miongoni mwa sababu nyingi alizozitoa ni pamoja na kusema kuwa mji wa Morogoro
ni ngome yao kubwa (ukiondoa Dar es Salaam) na hivyo safari hii wameupa heshima
ya kipekee.
Mara zote Jahazi imekuwa ikianza kutambulisha
nyimbo mpya jijini Dar es Salaam na baadae kufuatiwa na uzinduzi na baada ya
hapo ndio wanazipeleka nyimbo mpya mikoani.
Mauji pia katika mahojiano yake hayo alifichua
mikakati yao mikubwa ya kukukabiliana na ushindani kwa mwaka huu wa 2014.
